ALHAJI ADAM MASOUD MTOLE AWATAKA WANASIASA KUTOTUMIA AJALI YA GHOROFA LA KARIAKOO KWA MADHUMUNI YA KISIASA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Tuesday, 19 November 2024

ALHAJI ADAM MASOUD MTOLE AWATAKA WANASIASA KUTOTUMIA AJALI YA GHOROFA LA KARIAKOO KWA MADHUMUNI YA KISIASA

Alhaj Adam Masoud Mtole Awataka Wanasiasa Kutotumia Ajali ya Ghorofa la Kariakoo kwa Madhumuni ya Kisiasa



Na Paul Kayanda, Geita.


Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita, Alhaj Adam Masoud Mtole, amewaonya wanasiasa nchini kutotumia ajali ya ghorofa iliyoporomoka katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam kwa madhumuni ya kujipatia umaarufu au kujinufaisha kisiasa.


Akizungumza wakati akitoa salamu za pole kwa familia za wahanga wa ajali hiyo, Alhaj Mtole amesema kwamba ni muhimu kwa wanasiasa kuzingatia maslahi ya wananchi na kuwaonyesha mshikamano wakati wa majanga badala ya kutumia misiba kama fursa ya kufanya siasa za aina yoyote.


"Muda huu siyo wa kufanya siasa, bali ni wa kutoa msaada kwa wahanga na familia zao. Tunapaswa kuungana na wahanga katika kipindi hiki kigumu na kuwapa faraja, badala ya kutumia janga hili kujipatia faida kisiasa," alisema Alhaj Mtole.


Aidha, Mtole alitaja kuwa ni wajibu wa viongozi wa kisiasa kuwa na ustahimilivu na kujenga mazingira ya umoja na mshikamano, hususan wakati wa majanga ya kitaifa. Alhaj Mtole pia alikishukuru chama cha CCM kwa kuonyesha msaada wa haraka kwa wahanga wa ajali hiyo na akatoa wito kwa wananchi kote nchini kuendelea kutoa msaada na kushirikiana katika kusaidia wahanga wa ajali hiyo.


Mwisho, Mtole alisisitiza kuwa serikali inapaswa kuongeza juhudi za kuboresha miundombinu ya majengo na kuhakikisha usalama wa wananchi katika maeneo ya mijini, ili kuepuka majanga kama haya kwa siku zijazo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso