Na Paul Kayanda, Mbogwe
Wananchi wa kijiji cha Lwazeze kilichopo katika Kata ya Ngemo, wilayani Mbogwe mkoani Geita wameonesha uungwaji mkono mkubwa kwa Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, Mhe. Nicodemas Maganga, kwa kumchangia kiasi cha zaidi ya shilingi 200,000 kwa ajili ya kugharamia mchakato wa kuchukua fomu za ubunge kwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2025.
Hatua ya wananchi hao imekuja kutokana na mbunge huyo kuwa kivutio kwao cha maendeleo ya jimbo hili kwa kusimamia vizuri miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na fedha nyingi zinazoletwa na mhe.Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hasan.
Aidha wananchi hao wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema wameonyesha hisia zao kwa mbunge wao kwa kumtolea kiasi hicho cha fedha ili aingie tena kwenye kinyang'anyilo cha kugombea Ubunge kwani hawaoni mtu mwingine atakae waletea maendeleo lukuki ndani ya jimbo hilo.
"Mimi kama mwananchi wa kawaida pamoja na wenzangu, kwa kweli mbunge huyu anatufaa, ni miaka minne tu tumeona mafanikio makubwa katika jimbo,tulikuwa na mbunge na hatujawahi kuona maendeleo yoyote, akienda Dar anaishi na huko huko sisi wananchi anatusahau lakini Mbunge wetu Maganga kipindi kifupi tuna shule za sekondari na msingi za kutosha, Zahanati, Maji, umeme, na taa za barabarani pale Masumbwe, Barabara za lami, hatuwezi kuruhusu mtu mwingine apite hapa," alisema Mwasiti Ramadhani.
Mchango huu unaonyesha wazi jinsi wananchi wa Lwazeze wanavyothamini juhudi za Mheshimiwa Maganga katika kuboresha maisha ya wakazi wa jimbo la Mbogwe.
Katika kipindi cha utawala wake, Mheshimiwa Maganga ameweka jitihada kubwa katika kuleta maendeleo, hasa kwenye sekta za elimu, afya, miundombinu, na ustawi wa jamii.
No comments:
Post a Comment