TUZO ZA MALKIA WA NGUVU NI CHACHU YA MAENDELEO KWA WANAWAKE NA JAMII - DKT. BITEKO - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 5 April 2025

TUZO ZA MALKIA WA NGUVU NI CHACHU YA MAENDELEO KWA WANAWAKE NA JAMII - DKT. BITEKO



📌 Clouds Media yapewa heko miaka tisa ya Malkia wa Nguvu

📌 Clouds yaunga mkono jitihada za Rais Samia za kuwezesha wanawake kiuchumi


📌 Wanawake wasisitizwa kutumia Nishati Safi kulinda afya zao


Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati


Jukwaa la Malkia wa Nguvu la Clouds Media lilioanzishwa mwaka 2016 limeendelea kutimiza lengo lake la kuhamasisha na kuunga mkono wanawake katika nyanja za ujasiriamali, maendeleo ya kiuchumi na masuala mengine mbalimbambali ya kijamii kwa kipindi cha miaka tisa sasa.


Akizungumza Aprili 4, 2025 jijini Dar es salaam wakati aliposhiriki katika sherehe za Tuzo za Malkia wa Nguvu kwa mwaka 2025, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema jukwaa hilo pia hutambua, huthamini na husherehekea jitihada na michango ya wanawake waliothubutu na kufanikisha maendeleo katika nyanja mbalimbali za kijamii, uchumi na uongozi.


“ Tangu kuanzishwa kwake, hadi sasa, jukwaa hili limekuwa ni chachu kubwa ya maendeleo kwa wanawake na jami kwa ujumla. Naomba niwapongeze, Clouds Media Group kwa kazi hii nzuri. ” Amesema Dkt. Biteko


Amesisitiza “Kuanzisha na kuendeleza jukwaa hili ni kuunga mkono juhudi za Serikali na za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwawezesha wanawake kiuchumi, kuongeza ushiriki wao katika sekta mbalimbali na kuhamasisha maendeleo jumuishi, ”


Ametaja mafanikio ya Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake kijamii na kiuchumi sambamba na hatua kubwa ya kuhakikisha kuwa mwanamke anakuwa sehemu ya maendeleo katika jamii kuwa ni fursa za elimu, mazingira wezeshi ya kiuchumi, ushirikiano na jumuiya ya kimataifa, huduma bora za afya pamoja na huduma za maji safi na nishati ya kupikia.


Aidha, Dkt. Biteko ametoa rai kwa wadau wote muhimu kushirikiana na Serikali ili kutokomeza changamoto zinazohitaji kutatuliwa ili kufungua fursa zaidi kwa wanawake.


Vilevile ametoa wito kwa Clouds media na wanawake kushiriki kikamilifu katika kampeni mbalimbali za Serikali mfano Kampeni ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ili kuhakikisha wanawake wanatumia Nishati Safi na kuwa na afya salama.


Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kufikia malengo tarajiwa.


Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Mhe. Albert Chalamila amesema kuwa awali mwanamke hakuchuliwa kama kiumbe anayeweza kuwa na mafanikio makubwa duniani, hata hivyo hali imebadilika na sasa wanawake na Serikali mbalimbali duniani zimeonesha uwezo mkubwa wa wanawake katika sekta mbalimbali.


Mwenyekiti wa Kamati ya Malkia wa Nguvu kwa mwaka 2025, Lilian Masuka amesema kuwa Jukwaa la Malkia wa Nguvu imeweza kuwatunuku tuzo wanawake zaidi ya 70, na kuwatambua wanawake 300 katika shughuli zao.


Amesema katika mwaka 2025 wanatarajia kutembelea mikoa mitano, hivyo wanaiomba Serikali iwaunge mkono ili waweze kufika nchi nzima.


“ Kupitia Rais Samia tumeona uwekezaji mkubwa na sera zilizoboreshwa ili kusaidia wanawake kiuchumi ,” amesema Masuka.


Ameongeza kuwa wanawake wengi nchini bado wanatumia nishati isiyo safi ikiwemo mkaa, hivyo ametoa wito huo ili waweze kutumia Nishati Safi ya Kupikia pamoja na Serikali kuendelea kuwezesha mikopo rafiki kwa wanawake ili kuwawezesha kuwa na uwezo wa kumiliki vifaa vitakavyo wasaidia kutumia Nishati Safi ya Kupikia.


Kupitia sherehe hizo za tuzo za Malkia wa Nguvu 2025 wanawake mbalimbali wametambuliwa mchango na harakati zao katika jamii na kupatiwa tuzo.





MWISHO

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso