SERIKALI KUSUKUMA MAENDELEO YA AMCOS KWA NGUVU MPYA MKOANI SHINYANGA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 12 April 2025

SERIKALI KUSUKUMA MAENDELEO YA AMCOS KWA NGUVU MPYA MKOANI SHINYANGA



Serikali ya Mkoa wa Shinyanga imeweka mkakati wa kuimarisha vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) kwa lengo la kuvifanya kuwa na tija sawa na ile inayopatikana kwenye vyama vikuu vya ushirika vinavyofanya kazi kwa mafanikio makubwa mkoani humo.


Akizungumza katika Jukwaa la Ushirika lililofanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, amesisitiza umuhimu wa kuviwezesha vyama hivyo kuwa imara, endelevu na vyenye mchango mkubwa kwa wanachama na uchumi wa Mkoa.


RC Macha amewataka viongozi na wanachama wa vyama vya SHIRECU na KACU kuhakikisha wanadhibiti na kusimamia kwa uaminifu mali za wakulima ili kuhakikisha matokeo chanya yanapatikana hatua hiyo itasaidia kuhakikisha ushirika unatoa mchango halisi kwa ustawi wa wakulima na kuchangia pato la Mkoa na Taifa, pia amesema usimamizi bora wa rasilimali za wakulima ndio msingi wa mafanikio ya vyama hivyo.


Katika mkutano huo, RC Macha ametoa agizo kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Nyambi, kuitisha kikao maalum kitakachowajumuisha viongozi wa vyama vya msingi visivyopewa kipaumbele kama Chama cha Wafugaji na Wachimbaji wa Madini ambapo lengo la kikao hicho ni kujadili changamoto, kutafuta suluhu na kubuni mbinu mpya za kuboresha utekelezaji wa majukumu yao ndani ya Mkoa wa Shinyanga.


"Nakuagiza Mwenyekiti wa Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Shinyanga ndugu Nyambi, uandae kikao hicho ili tuweze kujadili changamoto na kuhakikisha kuwa utekelezaji wa majukumu unaendana na matokeo chanya kwa jamii na uchumi wa Mkoa kwa ujumla," amesema RC Macha.


Kwa upande wake, Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Shinyanga, Kakozi Ibrahim, alieleza umuhimu wa viongozi wa AMCOS kujitathmini kuhusu utendaji wao na uwajibikaji wao kwa wanachama huku akisema kuwa mafanikio au kushindwa kwa chama yanatokana moja kwa moja na ufanisi au udhaifu wa viongozi wake, hivyo ni muhimu kuwa na viongozi wenye maono, uadilifu na ufanisi.


Naye Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Emanuel Cherehani, alisisitiza umuhimu wa vyama vya ushirika kuandaa taarifa sahihi za fedha na matumizi kulingana na viwango vya kiuhasibu. 


Aidha, amewataka wanachama wote kuzingatia kanuni na maadili ya ushirika ili kuhakikisha vyama hivyo vinadumu na kuleta tija kwa wanachama na jamii kwa ujumla.


Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Ushirika Hujenga Ulimwengu Uliyo Bora”.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso