Na Berensi China
Zaidi ya wananchi 10,000 wa vijiji vya Kata ya Sakwe, Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama kwa muda mrefu, sasa wameondokana na adha hiyo kufuatia ujenzi wa mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).
Mradi huo ambao umegharimu zaidi ya shilingi bilioni moja, umeelezwa kufikia asilimia 78 ya utekelezaji. Akitoa taarifa kwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa, Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Bariadi, Mhandisi Hery Magoti, alisema tayari mkandarasi amelipwa kiasi cha shilingi 653,462,252. Aliongeza kuwa mradi huo unahusisha uchimbaji wa kisima kirefu pamoja na ujenzi wa tanki kubwa lenye ujazo wa mita za ujazo 135.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Kenani Kihongosi, aliipongeza serikali kwa hatua hiyo kubwa ya maendeleo na kuwataka wananchi kuulinda miundombinu ya mradi huo ili udumu kwa muda mrefu. Alisisitiza umuhimu wa kushirikiana na vyombo vya usimamizi katika kuhakikisha hakuna uharibifu unaotokea.
Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu, Bi. Eva Degereki, alieleza kuwa mradi huo una manufaa makubwa kwa wananchi, hususan wanawake ambao walikuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta maji. Alisema RUWASA imetimiza kwa vitendo kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya "Kumtua Mama Ndoo Kichwani."
Mwisho
No comments:
Post a Comment