Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SACP) Janeth Magomi
NA NEEMA NKUMBI - KAHAMA
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linamshikilia dereva wa gari la mizigo lenye namba za usajili T552 BQN, mali ya kampuni ya CIMC, Ally Mohamed (41), kwa tuhuma za kumgonga mtembea kwa miguu, ambaye hakufahamika mara moja, na kumsababishia kifo chake katika eneo la Shunu, Kata ya Nyahanga, Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga.
Akizungumza kwa njia ya simu, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SACP) Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva huyo, ambaye alishindwa kuchukua tahadhari kwa watumiaji wengine wa barabara, licha ya kuwepo kwa alama za usalama barabarani (Zebra).
Shuhuda wa ajali hiyo, Bi. Esta, ameeleza kuwa mtu huyo ambaye hakufahamika mara moja alikuwa amesimama pembeni ya barabara na kujirusha kwenye uvungu wa gari, hivyo kugongwa na tairi za nyuma na kusababisha kifo chake.
Shuhuda mwingine, John Paul, ameeleza kuwa mtu huyo alikuwa amelala barabarani majira ya saa 4 asubuhi, aliondolewa na kupumzika pembeni ya barabara, kisha alijirusha mbele ya gari saa 10 jioni.
Afisa Muuguzi wa kitengo cha afya ya akili katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama, Boniface Isaiah, ameongeza kuwa matatizo ya afya ya akili yanaweza kusababisha mtu kujihatarisha, na magonjwa ya muda mrefu kama kisukari na ukimwi yanaweza kuchangia kwa asilimia 40 matatizo ya afya ya akili ambayo yanapelekea watu kujinyonga, kunywa sumu, au kuhusika katika ajali.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limesema linaendelea kufanya juhudi za kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara katika maeneo mbalimbali mkoani humo, hasa maeneo ambayo yanaripotiwa kuwa na ajali nyingi.
Kamanda Magomi amewataka madereva kuzingatia sheria na taratibu za usalama barabarani ili kuepuka ajali.
No comments:
Post a Comment