BINTI AFARIKI DUNIA KUFUATIA MAFURIKO YA MVUA KUBWA KAHAMA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday, 7 April 2025

BINTI AFARIKI DUNIA KUFUATIA MAFURIKO YA MVUA KUBWA KAHAMA

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, akitembelea maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko


NA NEEMA NKUMBI- HUHESO DIGITAL KAHAMA


Binti anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 16 hadi 19, ambaye hajafahamika jina wala makazi yake, amefariki dunia baada ya kusombwa na mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha tarehe 6 Aprili, 2025, majira ya saa 11 jioni katika Wilaya ya Kahama.


Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu tarehe 7 Aprili 2025, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga, Janeth Magomi, amethibitisha kifo hicho na kusema kuwa chanzo cha kifo cha mwanamke huyo ni mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha kwa masaa mawili mfululizo.


“Jana, Aprili 6, majira ya saa 11, mvua kubwa ilinyesha kwa masaa mawili mfululizo katika Wilaya ya Kahama, hali iliyosababisha maafa. Mara baada ya askari polisi wa Wilaya ya Kahama kupata taarifa za kifo cha mwanamke huyo ambaye anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 16 hadi 19, walifika kwenye eneo la tukio kwa lengo la kuchunguza zaidi,” amesema RPC Magomi.


Kamanda Magomi ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari na kuwa waangalifu wanapopita katika maeneo yanayopitia mvua kubwa.


Mmoja wa wananchi waliokumbwa na mafuriko, Rabia Edward, amesema kuwa maji yaliingia ndani ya nyumba na kufikia usawa wa kiunoni, huku yakiharibu vitu vyao kama magodoro na masofa.


Mwananchi mwingine, Juma Huseni, ameeleza kwamba ukosefu wa mitaro ya maji ni chanzo kikubwa cha mafuriko na kuomba serikali kuweka mitaro ili kusaidia kupunguza kasi ya maji.


Meneja wa Tarura Wilaya ya Kahama ameeleza kuwa maji hayawezi kuzuiwa, na kwamba ni muhimu maji yapite katika njia yake asili ili kuepusha kuharibika kwa miundombinu ya maji pia ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuacha maji yapite bila kuzuia ili kuepusha madhara zaidi.


Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, alipotembelea maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko, ameitaka idara ya ujenzi kutoa vibali vya ujenzi na kufuatilia maeneo ambayo wananchi wanajenga ili kuepusha ujenzi holela, huku akiongeza kuwa changamoto kubwa katika Wilaya ya Kahama ni ujenzi holela ambapo asilimia 75 ya ujenzi ni holela na asilimia 25 ni miundombinu inayohitajika.




No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso