BARAZA LA MADIWANI MANISPAA YA KAHAMA LATAKIWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO KABLA YA UCHAGUZI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday, 16 April 2025

BARAZA LA MADIWANI MANISPAA YA KAHAMA LATAKIWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO KABLA YA UCHAGUZI

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kahama, Andrew Chatwanga akizungumza katika baraza la madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama

NA NEEMA NKUMBI - HUHESO DIGITAL KAHAMA.


Viongozi mbalimbali wametoa wito kwa madiwani kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kikamilifu kabla ya kuelekea kwenye kipindi cha uchaguzi.


Wito huo umetolewa leo Aprili 16, 2025 katika Baraza la madiwani lililofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama.


Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kahama, Andrew Chatwanga, amewataka madiwani kutoingia “homa ya uchaguzi” na kusahau kutimiza majukumu yao waliyopewa na wananchi, huku akiwakumbusha kufanyia kazi maeneo ambayo bado hayajakamilika ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inakamilika kwa wakati.


Chatwanga amesisitiza umuhimu wa kusimamia miradi ya barabara kwa ufanisi, hasa kwa kuzingatia changamoto za mvua zinazoendelea kuleta kero za mafuriko kwa wananchi aidha, amevitaka vyama vya upinzani kushirikiana na vyama vingine katika kuleta maendeleo kwa wananchi wote wa Kahama.


Kwa upande wake, Afisa Uchaguzi wa Jimbo la Kahama Mjini, Elkana Shija, amesema maandalizi ya zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yanaendelea pia amewataka wananchi kujitokeza kukagua taarifa zao pamoja na za ndugu zao, hata wale waliokwisha fariki waende kuzifuta ili kuhakikisha taarifa zinabaki katika usahihi huku akieleza kuwa Zoezi hilo litaanza rasmi Mei 1 hadi 7, 2025.


Mwenyekiti wa Chama cha CUF Wilaya ya Kahama, Dauda Hassan, ametoa rai kwa wasimamizi wa uchaguzi kutekeleza majukumu yao kwa haki na kwa kumcha Mungu, akisisitiza kuwa "Mungu husikia sala za waadilifu", Pia amewakumbusha madiwani kutekeleza ahadi walizotoa kwa wananchi wao.


Naibu Meya wa Manispaa ya Kahama, Wiliam Sindano, amesema kuwa kama ujenzi wa mzunguko (roundabout) katika eneo la Lumambo umeshindikana, basi eneo hilo liangaliwe kwa kuwekwa taa za barabarani kutokana na idadi kubwa ya ajali zinazotokea hapo.


Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Fabian Kamoga, amewapongeza madiwani kwa juhudi wanazofanya katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa baraza pia amewasihi kuhakikisha wanakamilisha majukumu yao ipasavyo kabla ya baraza kufungwa rasmi.



Akihitimisha kikao hicho, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani ambaye pia ni Naibu Meya, Wiliam Sindano, amemuomba Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kahama kusaidia katika kukamilisha viporo vya miradi iliyobaki ili madiwani wasikumbane na maswali magumu kutoka kwa wananchi wakati wa uchaguzi.





No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso