Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema hakuna atakayezuia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.
NA NEEMA NKUMBI- HUHESO DIGITAL
Akiwahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Manispaa ya Kahama mnamo Machi 27, 2025, Wasira amesisitiza kuwa licha ya kampeni za upinzani, hakuna atakayekuzuia uchaguzi, kwani tayari hatua za awali za maandalizi ya uchaguzi zimeanza, ikiwemo kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura katika mikoa mbalimbali ya Tanzania.
“Hawa wanaoogopa uchaguzi wanajua kuwa wakija, mtawapiga chini ndiyo maana wanazungumza kuhusu mabadiliko na kuzuia uchaguzi, lakini hawawezi kuzuia uchaguzi, Katiba inasema kuwa uchaguzi wa Tanzania unaweza kuahirishwa tu ikiwa kuna vita, sasa nauliza, huku Kahama kuna vita?” amesisitiza Wasira.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Richard Kaselela, amezungumzia hali ya wachimbaji wadogo wa madini, akisema kuwa wamiliki wa mashamba katika sekta ya madini wameachwa nyuma na kuendelea kuwa masikini, huku wachache wakijengewa utajiri ambapo amehimiza kwamba serikali iangalie maslahi ya wachimbaji wadogo na kuhakikisha wanafaidika na sekta hiyo.
“Kama tunao wawekezaji, tuwaangalie na wafaidi pamoja na wenzetu, Nia njema ni kuhakikisha kila mtu anafaidika,” amesema Kaselela.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mabala Mlolwa, amesisitiza kuwa sekta ya madini inahitaji maboresho ili wachimbaji wadogo waendelee kunufaika, na ameongeza kuwa Shinyanga bado ni ngome imara ya CCM.
Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, ameiomba serikali kuongeza idadi ya mameneja wa TARURA katika Halmashauri ili kuboresha usimamizi wa miradi ya barabara.
No comments:
Post a Comment