Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Shinyanga wametakiwa kuwa chanzo cha kutatua kero za wananchi katika maeneo yao, na kuepuka kuwa vyanzo vya migogoro.
Haya yamesemwa march 10, 2025 na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM mkoa wa Shinyanga, John Siagi, aliyemuwakilisha Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Tanzania Ally Hapi, katika tamasha la kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa utekelezaji bora wa Ilani ya CCM 2020-2025.
Siagi amesema viongozi hao wanapaswa kuendelea kuwajibika kikamilifu katika majukumu yao ili wawe mfano wa kuigwa katika jamii kwa utekelezaji wa Ilani ya chama cha Mapinduzi katika miradi mbalimbali ya maendeleo, na si kuwa sehemu ya kunyoshewa vidole.
"Unapokuwa chanzo cha migogoro kwa unaowaongoza, unafikiri wanakufikiriaje au wanakuchukuliaje? Tunapaswa kuwa watu na kupigiwa mifano kwa kuwa viongozi bora na siyo watu wa kunyooshewa vidole, na hiyo ndiyo dhamira ya Mwenyekiti wetu wa Chama, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan," amesisitiza Siagi.
Katika hafla hiyo, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Kahama, Felix Bwahama, ameeleza kuwa sherehe hiyo ilikusudiwa kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imeleta mabadiliko makubwa, ikiwemo maboresho katika miundombinu ya usafiri.
"Tumezoea watu walikuwa wakisafiri kutoka Bukoba kwenda Dar es Salaam kwa wiki nzima, lakini sasa unasafiri na kufika siku hiyo hiyo kutokana na ubora wa miundombinu inayoendelea kujengwa na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan," amesema Bwahama.
Naye, Katibu wa CCM Wilaya ya Kahama, Andrew Chatwanga, amewataka viongozi wa kata kuacha tabia ya kuwafukuza makatibu wa matawi na mabalozi, na badala yake wawafukuze wanaovunja utaratibu wa chama kwa kuanza kupita kwa wajumbe kabla ya uchaguzi mkuu.
"Wapo watu wanahitaji kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, ni haki yao, lakini wasubiri kwanza Filimbi ipigwe. Hatuwezi kuendelea na zoezi la kuchagua viongozi kabla ya wakati. Uchaguzi wa mwaka huu utakuwa tofauti na wa miaka mingine, tutampa fomu yeyote anayetaka kugombea, halafu sisi uongozi wa wilaya na mkoa tutawachuja," ameeleza Chatwanga.
Katibu wa Baraza la Wazee Nchini, Underson Lymo, ameeleza kuwa wazee wanashukuru serikali kwa kuboresha huduma za matibabu, na kusema kuwa hili ni jambo muhimu ambalo linawafanya wazee kuwa na heshima kubwa kwa serikali.
No comments:
Post a Comment