NA NEEMA NKUMBI HUHESO DIGITAL - KAHAMA
Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wametakiwa kuwa wamoja na kushirikiana kwa karibu pia kusajili wanachama wapya na kuimarisha jumuiya yao kwa lengo la kujenga chama imara.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa, katika baraza la vijana Mkoa wa Shinyanga lililofanyika Machi 15, 2025, katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama.
Mlolwa amesema kuwa, huu sio muda wa kufukuzana au kutoa watu katika nyadhifa mbalimbali walizonazo, bali vijana wanapaswa kuvumiliana wakati wa changamoto na kuzungumza kwa pamoja ili kuzitatua.
“Vijana mna nafasi kubwa ya kulitumikia taifa. Huu sio muda wa kumfukuza kiongozi kutoka wadhifa alionao, bali ni wakati wa kukaa mezani tuongee na kama kuna kiongozi mwenye changamoto, ajadiliwe kwanza katika jumuiya yake na si kutolewa bila kujua kutoka kwa jumuiya,” alisema Mlolwa.
Pia, amewataka vijana kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi huu, na iwapo watashindwa, wawe na kifua kipana na kuweza kustahimili changamoto zote.
Akisoma taarifa ya umoja wa vijana CCM, Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Naibu Katalambula, amesema hadi sasa Mkoa wa Shinyanga una wanachama wa UVCCM 169,426, waliosajiliwa kielektroniki na kulipa ada, na mkakati wao ni kuendelea kusajili wanachama zaidi.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Shinyanga, Benard Werema, amesema kuwa kulikuwa na changamoto ya baadhi ya vijana kutolewa katika nyadhifa zao, lakini anashukuru kuwa uongozi wa CCM umesikiliza na kutatua changamoto hiyo, na sasa vijana wamerudishwa na chama kiko salama.
Werema pia ameeleza kuwa azimio la jumuiya ya vijana ni kuunga mkono Azimio la Mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliofanyika tarehe 18 na 19 Januari 2025 jijini Dodoma, ambalo lilipitisha wagombea wa Chama kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Vijana wa CCM Mkoa wa Shinyanga wamesema wapo tayari kuhakikisha ushindi mkubwa wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa kuhamasisha ushiriki wa vijana katika uchaguzi na kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kushiriki kupiga kura.
“Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Shinyanga tunathibitisha kwa kauli moja kuwa tutahakikisha CCM inapata ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa 2025. CCM Daima – Vijana ni Nguvu ya Ushindi!”

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa, akizungumza katika baraza la vijana Mkoa wa Shinyanga lililofanyika Machi 15, 2025

Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Shinyanga, Benard Werema akizungumza katika baraza la vijana Mkoa wa Shinyanga lililofanyika Machi 15, 2025

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa, akiwa katika picha ya pamoja na vijana wa Uvccm mara baada ya kuhitimisha baraza la vijana

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa, akivalishwa skafu na vijana wa Uvccm Mkoa wa Shinyanga

Katibu Uhamasishaji na Chipukizi UVCCM Mkoa wa Shinyanga Arnold Bweichum akizungumza katika baraza la vijana Mkoa wa shinyanga lililofanyika machi 15, 2025.
No comments:
Post a Comment