📌 Dkt. Biteko afanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Barbados
📌 Wakubaliana kuwekeza katika Ushirikiano Sekta ya Utalii na Maji
📌 Nishati Safi ya Kupikia, M300 kivutio cha mazungumzo
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Barbados, Mhe. Mia Mottley ambapo wamekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika makazi rasmi ya Waziri Mkuu, Mhe. Mia Mottley, Jijini Bridgestone, nchini Barbados.
Waziri Mkuu Mia amesema, kuna umuhimu wa kuwa na mkakati wa pamoja na kushirikiana kwa lengo la kukuza utalii kati ya Barbados na Tanzania na nchi za Afrika Mashariki kwa ujumla. Amesema kuna maeneo mengi ya vivutio vya utalii ambavyo vinaweza kuzinufaisha pande hizo mbili yakiwemo masuala ya ukarimu.
Maeneo mengine ya ushirikiano ni katika utoaji wa mafunzo maeneo ya ufundi kati ya nchi za Carib (Caribbean) na nchi mbalimbali za kiafrika huku akisisitiza kuwa umuhimu wa uboreshaji wa masoko na kubadilishana wataalam katika sekta mbalimbali kwa makubaliano maalum.
Aidha, amesema upo uhitaji wa wataalam katika sekta ya maji na miundombinu na hivyo kuna uwezekano wa kubadilishana wataalam ili kujengeana uzoefu katika sekta mbalimbali kulingana na makubaliano yatakayofikiwa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Biteko amesema mapendekezo hayo ni mazuri na yanaweza kuwa matokeo chanya baada ya kuchambuliwa na watalaam katika sekta husika kupitia Wizara zinazohusika na masuala ya kidiplomasia.
Dkt. Biteko amesema Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendeleza kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia ambayo inalenga kuwawezesha asilimia 80 ya watumiaji wa nishati kuondokana na matumizi ya nishati isiyokuwa safi ifikapo mwaka 2034.
Katika utekelezaji wa mpango huo, amesema Tanzania inatembea kifua mbele kunadi mkakati huo wa miaka 10 ambao pamoja na mambo mengine unakusudia kupunguza madhara kwa watumiaji wa nishati isiyokuwa safi inayopelekea uchafuzi wa mazingira, magonjwa ya kupumua pamoja na vifo.
“Januari mwaka huu tumekuwa na mkutano wa Wakuu wa nchi za Afrika (M300) uliofanyika jijini Dar es Salaam ukilenga kuwa wezesha watu milioni 300 barani Afrika ambao hawajaona umeme kuweza kupata haki hiyo ikiwa ni miaka mitano kuanzia sasa na baada ya hapo itaweka namna tunavyoweza kusonga mbele kulingana na matokeo yanayofikiwa” amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko amefafanua kuwa, hatua ya Tanzania kushiriki katika mkutano wa nishati endelevu kwa wote (SEforALL) uliofanyika nchini Barbados, ni kuthibitisha nia yake thabiti inayolenga matokeo chanya. Hivyo, amesema yapo maeneo mengi ya kushirikiana na kuwezesha wananchi wa pande zote mbili kupata maendeleo na ustawi wa pamoja.
Mkutano wa Dkt. Biteko Waziri Mkuu wa Barbados, umehitimisha ziara ya kikazi nchini humo ambako alishiriki katika Kongamano la kimataifa la nishati endelevu kwa wote pamoja na mikutano ya wadau mbalimbali iliyojikita katika uboreshaji wa sekta ya nishati kwa manufaa ya nchi hizo mbili.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, alifuatana na Waziri wa Maji, Nishati na Mhe. Shaib Kaduara, Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Humphrey Polepole, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mha. Felichesmi Mramba na Mshauri wa Rais katika masuala ya Nishati na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Angellah Kairuki.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment