Na Berens China Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi, amewataka wananchi wa Kata ya Nyakabindi, halmashauri ya Mji wa Bariadi, kuutunza mradi wa maji ambao umeghalimu zaidi ya shilingi milioni 400, na ambao unatarajiwa kutatua kero ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wa kata hiyo.
Kihongosi alisisitiza umuhimu wa kulinda miundombinu ya maji ili kuhakikisha kuwa mradi huo unadumu kwa muda mrefu na kuwa na manufaa kwa vizazi vijavyo. Alisema kuwa serikali imekuwa ikitumia pesa nyingi katika kutekeleza mradi huo, hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha kuwa miundombinu hiyo inatunzwa.
Kwa upande mwingine, Katibu wa CCM wa Mkoa wa Simiyu, Eva Degereck, alisema kukamilika kwa mradi huo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM na pia ni ishara ya dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama kichwani kwa kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma za msingi, ikiwemo maji, kwa urahisi.
Diwani wa Kata ya Nyakabindi, Alias Masanja, alisema kuwa mradi huo umeleta mabadiliko makubwa kwa wananchi wa kata hiyo, ambao tangu uhuru walikuwa wakitembea zaidi ya kilometa 30 kutafuta maji. Alisema kuwa sasa, wananchi hawawezi tena kusafiri umbali mrefu, kwani mradi wa maji umekuja kuwaondolea kero hiyo kubwa.
Wananchi wa Kata ya Nyakabindi, wakiwemo akina mama, walipongeza serikali kwa kuleta mradi huo ambao umeondoa adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji. Walielezea furaha yao na shukrani kwa serikali kwa kutoa suluhisho la kudumu kwa tatizo la maji.
Awali, akizungumza kwa niaba ya Mhandisi wa RUWASA Bariadi, Mhandisi Helli Magoti alieleza kuwa kukamilika kwa mradi huu kutasaidia kupunguza maradhi yanayotokana na ukosefu wa maji safi na salama.
Alisema zaidi ya wananchi 400,000 wanatarajia kunufaika na mradi huu, ambao utatoa suluhisho la kimsingi la upatikanaji wa maji safi na salama kwa jamii ya Nyakabindi.
No comments:
Post a Comment