PIC YAITAKA WIZARA YA UJENZI NA TANROADS KUIMARISHA USIMAMIZI KWA CHICO ILI UWANJA WA NDEGE UKAMILIKE HARAKA. - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Thursday, 20 March 2025

PIC YAITAKA WIZARA YA UJENZI NA TANROADS KUIMARISHA USIMAMIZI KWA CHICO ILI UWANJA WA NDEGE UKAMILIKE HARAKA.


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Augustino Vuma (MB) imeiagiza Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Shinyanga kumsimamia Mkandarasi China Henan International Cooperation Group Co. Ltd (CHICO) anayetekeleza upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Ibadakuli kuhakikisha kazi zilizobaki zinakamilishwa kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa ili kuleta tija ya miradi inayotekelezwa na Serikali.


Maagizo hayo yametolewa leo Machi 20, 2025 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Augustino Vuma baada ya kutembelea na kukagua Utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Ibadakuli kilichopo Manispaa ya Shinyanga, mradi unaogharimu Tzs. Bilioni 48 na ambao mpaka sasa umefikia asilimia 75% ya utekelezaji wake.


“Kamati inaiagiza Wizara ya Ujenzi na TANROADS mkoa wa Shinyanga kumsimamia Mkandarasi (CHICO) kwa ukaribu ili kuhakikisha kazi zote zilizobakia kwenye mradi huu zinakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia ubora ili kuleta tija kwenye miradi ambayo inatekelezwa na Serikali na hatimaye wananchi ambao ndio wanufaika wakubwa wafurahie matunda yake”, amesema Mhe. Augustino.


Aidha Kamati imeiagiza Wizara ya Ujenzi, TANROADS Mkoa wa Shinyanga pamoja na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kushirikiana kwa pamoja ili kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa alipotembelea Uwanja huu wa Ndege na kuagiza uwanja uanze kutumika wakati wakisubiri jengo la abiria likamilike.


Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Dkt. Charles Msonde, amekiri kupokea maelekezo na ushauri wa Kamati na kuahidi kuwa watafuata maelekezo yote ikiwa ni pamoja na kumsimamia mkandarasi ili kuhakikisha utekelezaji wa mradi huu unakuwa wenye tija na unakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Julius Mtatiro (Wakili) akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha, ameishukuru kamati kwa kutoa maelekezo haya kwani huu uwanja utakapoanza kutumika utakuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi mkoani Shinyanga kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazofanyika kama kilimo, biashara na madini, pia utaimarisha mtandao wa usafiri wa anga nchini lakini pia utakuwa kivutio kikubwa na kutokeza fursa kwa wafanyabiashara na wawekezaji kuja mkoani hapa.


Mradi huu unahusisha ujenzi wa barabara ya kilomita 2 ya kuruka na kutua ndege, maegesho ya ndege, jengo la abiria, mnara wa kuongozea ndege, maegesho ya magari nk. ambapo uwanja utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kupokea ndege za ukubwa wa aina ya Bombardier Q400.


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso