MVUA YA UPEPO MKALI YAANGUSHA KANISA LA MLIMA WA MOTO KAHAMA WANANCHI WAMWANGUKIA MKUU WA MKOA SHINYANGA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday, 21 March 2025

MVUA YA UPEPO MKALI YAANGUSHA KANISA LA MLIMA WA MOTO KAHAMA WANANCHI WAMWANGUKIA MKUU WA MKOA SHINYANGA



Na Paul Kayanda, Kahama

MVUA kubwa iliyoambatana na upepo mkali imenyesha na kuleta athari kubwa katika Kitongoji cha Mwagala, Kijiji cha Igung'hwa, Kata ya Kinaga, Manispaa ya Kahama, Mkoani Shinyanga, na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali.


Miongoni mwa madhara makubwa ni kuanguka kwa paa la Kanisa la Mlima wa Moto, tukio hilo limesababisha hofu kubwa miongoni mwa waumini wa kanisa hilo na wananchi wa kitongoji hicho kwa ujumla.


Mchungaji wa kanisa hilo, Moses Shihanda, alisimulia jinsi mmoja wa waumini hao alivyonusurika kifo baada ya paa la kanisa hilo kuanguka kutokana na mvua iliyoambatana na upepo mkali huku muumini wake ambaye hakupenda kutaja jina lake akiwa ndani ya kanisa. Jitihada za kumnasua ziluzaa matunda baada ya wasamaria wema kujitokeza kwa wingi.


Aidha, Mchungaji Shihanda amesema kuwa tukio hilo lilitokea juzi kuanzia majira ya saa nne usiku ambapo ilinyesha mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali pamoja na ngurumo za radi kali, na kusababisha madhara kwenye kanisa lake pamoja na nyumba ya ofisi ya kanisa.


"Hasara ambayo kanisa limepata, ingawa hatujafanya tathmini kamili, ni zaidi ya viti 30 vilivyoharibiwa, vifaa kwa ajili ya matumizi ya kanisa, nyaraka mbalimbali, kanisa lenyewe, nyumba ya ofisi, na vitu vingine vimekandamizwa kama vifaa vya muziki, na uokoaji unaendelea ili kubaini hasara kwa ujumla," alisema Moses Shihanda.


Wananchi wa eneo hilo walielezea masikitiko yao kuhusu tukio hilo, huku wakisema baadhi yao walikosa makazi kutokana na mvua hiyo iliyonyesha juzi, ikijumuisha upepo mkali jambo ambalo walisema serikali inapaswa ichukue hatua za haraka kusaidia wananchi wake kwani kwa sasa kwa kanda ya ziwa hususani Mikoa y Shinyanga, Mwanza, Geta na Simiyu mvua zinazonyesha ni zile zenye athari kwa wananchi.


Pia walisema kuwa hali hii imewaathiri kiuchumi na kijamii, na kupelekea ombi la msaada kutoka kwa viongozi wa serikali walichukulue suala hilo kwa uzito mkubwa.


Viongozi wa vijiji na kitongoji hicho wameiomba Kamati ya Maafa ya Wilaya, inayooongozwa na Mkuu wa Wilaya Mboni Mhita, kufika katika eneo hilo ili kujionea na kutoa pole pamoja na kusaidia katika juhudi za kurejesha hali ya kawaida.


Kamati za maafa katika mikoa na wilaya zimehimizwa kujipanga na kuweka mipango ya dharura ili kukabiliana na maafa kama haya, kama ilivyoelekezwa na aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama.


Pamoja na mambo mengine, wananchi wa maeneo hayo walisema kuwa wanaamini Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, watafika kujiludhisha kwa kuwa wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa pole na kuhamasisha juhudi za pamoja za kukabiliana na madhara ya maafa.


Wananchi hao walisema kuwa mbali na kanisa hilo kuanguka, pia wapo wananchi ambao hawana makazi ya kueleweka kutokana na janga hilo la mvua iliyoambatana na upepo mkali. Hata kanisa la Waadiventista Wasabato kilichopo katika kitongoji hicho nalo limeezukiwa paa.


Naye mwenyekiti wa kitongoji cha Mwagala pamoja na mjumbe wa serikali ya kijiji cha Igung'hwa walisema wameomba serikali kupitia Kamati ya Maafa Wilaya pamoja na wananchi wenye moyo kujitolea misaada kwa wahanga hao ili kurejesha hali ilivyokuwa kwa wananchi wao.


Katika hatua nyingine wananchi wa kata ya majengo manispaa ya Kahama wameiomba serikali kuchukua hatua madhubuti ya kuendeleza ujenzi wa mtaro mkubwa eneo la Cafe Latino unaomwaga maji kwenye makazi ya wananchi na kuleta athari mbalimbali.


"Tumechoka kuzoa maji ndani, kila mvua zinaponyesha wananchi tunaokaa hapa eneo la Cafelatino kila mvua zinapoanza kunyesha kama ni usiku tunakaa tongo macho ili tusife maji maana miaka mingi tunazoa maji hadi tunapata maradhi na Huyo Dc kila masika anakuja kututembelea na hali bado ipo vile vile," alisema mwananchi huyo bila kutaja jina lake kwa kuhofia usalama wake.


Mwananchi mwingine aliyekuwa akichota maji yaliyoingia ndani aligoma kutoa ushirikiano kwa mwandishi wa habari hizi kwa kile alichodai kuwa serikali ya wilaya miaka yote imegoma kuchonga mtaro mkubwa utakayopeleka maji huko bwawa lyanzungu kama ilivyodai ili kunusuru maji ya m ua kuingia kwenye makazi yao jambo ambalo halitekelezeki.


Hali ya sasa inahitaji ushirikiano wa karibu kati ya wananchi, viongozi wa serikali, na kamati za maafa ili kuhakikisha usalama na ustawi wa jamii katika maeneo yanayokumbwa na maafa.


Mwisho.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso