Afisa mauzo na masoko wa kampuni ya Magic Biulders International Derick Mmassy, akizungumza wakati wa zoezi la kuchangia damu katika hospitali ya Manispaa ya Kahama.
Na Mwandishi wetu Kahama.
Kampuni ya Magic Builders International ltd wazalishaji na wasambazaji wa vifaa mbalimbali vya ujenzi, imeungana na mafundi ujenzi wilayani Kahama mkoani Shinyanga kuchangia damu katika hospitali ya Manispaa ya Kahama, katika kuunga mkono jitihada za serikali, katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za Afya kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, afisa mauzo na masoko wa kampuni hiyo kanda ya ziwa Derick Mmassy amesema, lengo la kushiriki zoezi hilo ni kuokoa maisha ya wenye uhitaji wakiwemo kinamama wajawazito, kabla na baada ya kujifungua, watoto chini ya miaka mitano, wahanga wa ajali, pamoja na wahitaji wengine.
Mmassy ametoa wito kwa vikundi/taasisi na watanzania wenye mapenzi mema na kujitokeza kuchangia damu kama walivyofanya mafundi ujenzi hao kupitia chama cha mafundi ujenzi Kahama – CHAMAUKA.
“Tuko hapa kama Magic Builders International ltd kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mpango wa damu salama tuko hapa pia kuwaunga mkono wadau wetu wa ujenzi, mafundi wa Kahama, ambao kwa muunganiko wao wamewiwa kuja hapa kuchangia damu” Alisema Mmassy
Mwenyekiti wa chama cha mafundi ujenzi Kahama (CHAMAUKA), Baraka Moshi amesema wamefikia uamuzi huo wa kujitolea damu ili kuokoa maisha ya wenye uhitaji katika hospitali ya manispaa ya Kahama na vituo vya jirani.
Moshi ameomba serikali kupitia wadau mbalimbali wa Afya kutoa elimu kwa vijana kuhusu zoezi la uchangiaji wa damu kutokana na vijana wengi kutojitokeza wakihofia kupimwa maambukizi ya VVU na UKIMWI.
Amesema zaidi ya mafundi ujenzi 150 wamejitokeza katika zoezi hilo lililoendeshwa na chama hicho kwa kushirikiana na kampuni ya uzalishaji wa vifaa mbalimbali vya ujenzi ya Magic Builders International.
“Changamoto niliyokutana nayo ni mafundi wengi kuanza kuuliza hapa sasa tukienda kuchangia si tutapimwa ukimwi, lakini niliwahamasisha kama nilivyoelekezwa na wataalamu wetu kwamba, kwenye damu kule, utapimwa wingi wa damu na uzito , na vilevile damu itachukuliwa itaenda kupimwa kwenye maabara ya kanda, kwa hiyo majibu yale kama fundi atayahitaji atapewa maelekezo ya kwenda kuyachukua baadae” Alisema Moshi
Mmoja wa mafundi ujenzi kutoka chama cha mafundi ujenzi Kahama – CHAMAUKA, Mwasiti Issa amesema yeye binafsi amevutiwa na zoezi hilo na kujitolea kuchangia damu ili kuokoa maisha ya mama na mtoto kwani wamekuwa wahanga wakubwa wad amu.
Kwa upande wake mratibu wad amu salama katikaHalmashauri ya Manispaa ya Kahama Noel Malaki amewashukuru mafundi ujenzi hao pamoja na Magic Builders kwa moyo huo wa kujitolea kuchangia damu kwani uhitaji ni mkubwa katika hospitali hiyo.
Amesema mafundi hao wamechangia Unit 29 ambazo zitakwenda kuwasaidia wenye uhitaji baada ya taratibu kukamilika na kueleza kuwa Hospitali hiyo kwa siku inatumia unit 15 hadi 20 za damu, kwa mwezi ni unit 450 hadi 600, huku pia hospitali hiyo ikihudumia vituo vya Afya vinavyotoa huduma yad amu salama ndani ya manispaa hiyo nakusisitiza kuwa damu haiuzwi.
“Wito wangu kwa jamii, unapofika kwenye vituo vinavyotoa huduma hii yad amu salama, view vya serikali au vya kibinafsi kama utaambiwa kulipia damu naomba utoe taarifa haraka iwezekanavyo kwa namba yangu ambayo ni 0787 07 10 21, inapatikana wakati wote” Alisema Malaki
Hata hivyo, Magic Builders kama mlezi wa vyama vya mafundi ujenzi hapa nchini, siku ya Jumatatu Mrach 10 , 2025 wanatarajia kuzindua ofisi ya chama cha mafundi ujenzi wilaya ya Kahama kilichoanzishwa April mwaka 2024.
Ofisi hiyo itazinduliwa, chama cha mafundi ujenzi Kahama – CHAMAUKA, kitakabidhiwa kwa mkuu wa wilaya ya Kahama kwa utambuzi na utatuzi wa changamoto zao kwa ukaribu zaidi, ambapo shughuli hiyo itatanguliwa na maandamano ya amani ndani ya manispaa ya Kahama.
Mratibu wa damu salama Manispaa ya Kahama Noel Malaki akizungumza muda mfupi baada ya kumalizika kwa zoezi la kuchangia damu lilifanywa na mafundi ujenzi Kahama kupitia chama cha mafundi ujenzi Kahama (CHAMAUKA)
Mafundi ujenzi wakisubiri kwenye foleni kwa ajili ya kuchangia damu
Baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na kusambazwa na kampuni ya Magic Biulders International ambazo lazima ziwe na chapa ya "Magic Biulders"
MWISHO.
No comments:
Post a Comment