Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama cha Walimu Wilaya ya Kahama( Kahama Manispaa na Halmashauri ya Msalala)
NA NEEMA NKUMBI- HUHESO DIGITAL KAHAMA
Chama cha Walimu Wilaya ya Kahama, Mkoani Shinyanga, kupitia SAMIA TEACHERS MOBILE CLINIC, kimebaini kuwa walimu 890 hawapo katika vyeo wanavyostahili kutokana na ajira tofauti tofauti, ambapo Walimu 419 wapo katika Kahama Manispaa na 471 katika Msalala.
Haya yamebainishwa tarehe 25 Machi 2025 na Katibu wa Chama cha Walimu CWT Wilaya ya Kahama, Mwalimu Josias Paga, alipokuwa akisoma risala kwa mgeni rasmi ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita.
Mwalimu Josias ameeleza kuwa baadhi ya walimu walipandishwa vyeo tangu mwaka 2017, lakini hawajalipwa stahiki zao, hali inayosababisha usumbufu mkubwa, hasa kwa walimu waliostaafu au wanaotarajia kustaafu, hivyo kulipwa mafao pungufu.
Pia ameeleza changamoto zinazowakumba walimu, ikiwemo uhaba wa nyumba za walimu, hali inayowalazimu kuishi mbali na maeneo ya shule, Aidha amesema kuwa walimu wanakutana na changamoto ya kuhamishwa bila kulipwa stahiki zao za uhamisho kwa wakati, pamoja na kutopokea fedha za vikao kwa wakati.
Hata hivyo, Mwalimu Josias ameeleza mafanikio waliyoyapata, ikiwa ni pamoja na kununua vifaa vya kuwahudumia walimu, kama vile viti na matenti, pamoja na basi jipya aina ya TATA MARCOPOLO.
Pia amesisitiza umuhimu wa kliniki ya Samia Teachers Mobile Clinic iliyofanyika Februari 2025, ambayo ililenga kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili walimu, ikishirikiana na wizara zinazohudumia walimu, maafisa utumishi, na TSC Wilaya.
Walimu walimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua alizochukua, ikiwemo kupandisha vyeo stahiki kwa walimu kulingana na umri wao kazini, kuajiri walimu wapya 300 kwa shule za msingi na sekondari, pamoja na kuongeza asilimia ya mafao kutoka 33% hadi 40% kuanzia Julai 2024.
Akijibu risala hiyo, Mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, amesisitiza kuwa sekta ya elimu lazima ipewe kipaumbele ambapo amesema kuwa maelekezo kutoka kwa Rais Samia yamekamilika na kwamba wahusika wote, wakiwemo Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, wanafanya kazi kwa ushirikiano kuhakikisha sekta ya elimu inapata mafanikio makubwa.
“Mheshimiwa Rais Samia ametoa maelekezo kwa Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kwamba sekta ya elimu lazima ipewe kipaumbele, Niwahakikishie kuwa haya yanayoendelea siyo tu porojo, bali ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais,” amesema Dc Mboni.
Pia ameeleza kuwa atakutana na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya tatu ili kuendelea kuhamasisha na kuzingatia masuala ya elimu, ambapo amesisitiza kuwa walimu ni viongozi na wanajukumu muhimu katika jamii.
Hata hivyo Dc Mboni amewaahidi wajumbe hao kuwapeleka kwenda kutalii katika mbuga ya wanyama Serengeti.
Hadi sasa, Wilaya ya Kahama (Kahama Manispaa na Msalala) ina jumla ya walimu 3,054 walioungana na CWT, ambapo 2,930 ni wanachama na 124 si wanachama.
No comments:
Post a Comment