CHAMA CHA USHIRIKA MBOGWE NA BUKOMBE (MBCU) KUANZISHA MFUMO WA STAKABADHI KWA ZAO LA DENGU - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 29 March 2025

CHAMA CHA USHIRIKA MBOGWE NA BUKOMBE (MBCU) KUANZISHA MFUMO WA STAKABADHI KWA ZAO LA DENGU

 

Mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika Mbogwe na Bukombe Said Tangawizi akizungumza na wajumbe wa mkutano wa saba wa mwaka wa MBCU

NA NEEMA NKUMBI - HUHESO DIGITAL MASUMBWE, GEITA


Chama Kikuu cha Ushirika cha Mbogwe na Bukombe (MBCU) kinatarajia kuingiza zao la dengu katika mfumo wa stakabadhi ya mazao ghala, kwa kufuata maelekezo ya serikali, Lengo kuu ni kumsaidia mkulima kupata bei nzuri na pia kuimarisha ushirika kupitia mapato ya ushuru.


Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Mbogwe na Bukombe, Said Tangawizi, amesema kuwa licha ya kujihusisha na mazao kama Tumbaku na Pamba, sasa wameongeza zao la dengu katika shughuli zao za kilimo.


Hata hivyo, Tangawizi amebainisha changamoto mbalimbali zinazoikumba zao la dengu, ikiwa ni pamoja na walanguzi kuwapa wakulima fedha wakati wa kilimo, pindi mavuno yanapokuwa tayari waweze kuchukua mazao badala ya fedha na pia matumizi ya vipimo vikubwa visivyolingana na vipimo halisi.


Mkulima wa zao la dengu, Mayeju Kufungile Sangijo, ameipongeza hatua ya kuongeza zao hili kwa kusema linatoa ushindani kwa zao la tumbaku na linasaidia wakulima kupata fedha nzuri, Hata hivyo ameomba serikali kuongeza msaada kwa zao la alizeti, ambalo linalimwa kwa wingi lakini halipati msaada wa kutosha kutoka serikalini.


Sangijo pia ameiomba serikali kusaidia kuwapa mbegu bora, pembejeo, na viatilifu kama ilivyo kwa mazao mengine ya kibiashara kama pamba na tumbaku.


Aidha, Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Geita, Doreen Mwanry, amewasihi wakulima kuepuka kutumia vibaya mikopo wanayopewa kwa malengo mengine tofauti na yaliyokusudiwa, huku akitoa mfano katika zao la tumbaku, akisisitiza kuwa ikiwa mkulima amepewa fedha kwa ajili ya mbolea, basi fedha hizo zitumike kununua mbolea na si kwa matumizi mengine.


Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbogwe, Paul Fransis, amesisitiza umuhimu wa utawala bora na ushirikishwaji katika vyama vya ushirika, ambapo ameeleza kuwa vyama vingi vimekufa kutokana na kutokukaguliwa na kufunga hesabu vizuri, na pia baadhi ya viongozi wamekuwa wabadhirifu, wakikiuka kanuni na sheria za ushirika.


Pia, amekipongeza chama cha MBCU kwa mipango yake ya kujenga viwanda vya kuchakata mpunga, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza thamani ya mazao na kukuza uchumi wa maeneo husika.

Mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika Mbogwe na Bukombe Said Tangawizi akizungumza na wajumbe wa mkutano wa saba wa mwaka wa MBCU
Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbogwe, Paul Fransis, akizumgumza na wajumbe wa mkutano wa saba wa mwaka wa MBCU
Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Geita, Doreen Mwanry, akiwasihi wakulima kuepuka kutumia vibaya mikopo 
Meneja wa chama kikuu cha ushirika Mbogwe na Bukombe Paul Samwel akizungumza na wajumbe wa mkutano wa saba wa mwaka wa MBCU
Mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika Mbogwe na Bukombe Said Tangawizi akizungumza na wajumbe wa mkutano wa saba wa mwaka wa MBCU


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso