Na. Paul Kasembo, MSALALA DC
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewataka Maafisa Elimu Kata na Wakuu wa Shule za Sekondari mkoani Shinyanga kubandika orodha ya majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na shule ili kuwabaini wale ambao bado hawajiunga na hatua za kisheria zichukuliwe kwa wazazi ambao hawajawapeleka watoto wao shule.
RC Macha ametoa wito huo Machi 3, 2025 wakati akiweka Jiwe la Msingi katika Shule ya Sekondari Bumva iliyopo Kata ya Segese Halmashauri ya Wilaya ya Msalala ambapo ameendelea kutoa wito kwa wazazi kuwapeleka shule watoto wa kike na wa kiume badala ya kuwapeleka wakachunge ng’ombe.
“Ninawaagiza Maafisa Elimu Kata na Wakuu wa Shule za Sekondari wote mkoani Shinyanga kubandika orodha ya wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na shule ili tuwabaini wanafunzi ambao bado hawajajiunga na shule ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa wazazi ambao hawajawapeleka watoto shule”, amesema RC Macha
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kufanya kazi kubwa ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Elimu kwani alitoa takribani Bilioni 6 kwa ajiri ya ujenzi wa Shule 8 za Kata ili kuwawezesha wanafunzi kunufaika na elimu bora.
Akiwasilisha taarifa ya ujenzi, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mwl. Nyerere Kafuru Songora amesema ujenzi huu ulianza kutekelezwa Novemba 19, 2024 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Machi 10, 2025 ambapo wanafunzi wa Shule ya Mwalimu Nyerere, Segese na wanaokaa maeneo ya karibu wataanza kusoma mara moja kwani tayari shule hii imeshasajiliwa kwa namba ya usajili S. 6824.
Mradi huu wa ujenzi unatekelezwa kwa kutumia Mfumo wa Force Account ambapo mpaka sasa ujenzi umegharimu takribani Milioni 603 ukihusisha ujenzi wa Jengo la Utawala,Vyumba vya Madarasa, Jengo la Tehama na Maktaba, Vyoo na kichomea taka, Tanki la maji pamoja na Jengo la Maabara.
@ortamisemi
@msalaladc2023
#shinyanga_rs
No comments:
Post a Comment