WIZARA YA AFYA YAZINDUA MAFUNZO YA VITENDO KWA WAKUNGA KUBORESHA HUDUMA ZA DHARURA KWA AKINA MAMA NA WATOTO - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday, 17 February 2025

WIZARA YA AFYA YAZINDUA MAFUNZO YA VITENDO KWA WAKUNGA KUBORESHA HUDUMA ZA DHARURA KWA AKINA MAMA NA WATOTO

 

Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Saitore Laiza akizungumza katika ghafla ya uzinduzi wa mafunzo ya huduma za dharura kwa akina mama na watoto wakati wa ujauzito kujifungua na baada ya kujifungua.


NA NEEMA NKUMBI- HUHESO DIGITAL KAHAMA 


Wizara ya Afya, kwa kutambua umuhimu wa huduma za dharura kwa akina mama na watoto wakati wa ujauzito, kujifungua, na baada ya kujifungua, imezindua mafunzo ya vitendo kwa wakunga ili kuwaongezea maarifa na ujuzi katika kukabiliana na dharura zinazojitokeza wakati wa kujifungua.


Akizungumza leo february 17, 2025 katika hafla ya uzinduzi, Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Saitore Laiza, kwa niaba ya Waziri wa Afya Mheshimiwa Jenista Mhagama, ameeleza kwamba zaidi ya asilimia 30 ya watoto wachanga wanazaliwa nyumbani hivyo ni vyema wakunga wanaowasaidia huko nyumbani wapewe mafunzo pia.


Dkt. Laiza amesema, "Wizara inatambua mchango mkubwa wa wakunga, hivyo hakuna maisha bila wakunga, Tunatarajia kupitia mafunzo haya, kutakuwa na ongezeko la wakunga, jambo linalolenga kupunguza vifo vya akina mama na watoto na kuboresha afya ya jamii kwa ujumla."


Akisoma hotuba ya Chama cha Wakunga Tanzania, Dkt. Beatrice Mwilike amesema kwamba licha ya mchango mkubwa wa wakunga katika huduma za mama na mtoto, nchini Tanzania bado hakuna programu ya moja kwa moja ya ukunga kama inavyotakiwa na Shirikisho la Kimataifa la Wakunga (ICM).

Dkt. Beatrice ameeleza kuwa ili kupata shahada ya ukunga, inawalazimu wanafunzi kusoma stashahada ya uuguzi, jambo linalosababisha wakunga kutotimiza malengo yao kwa wakati.


"Tunaiomba serikali iruhusu vyuo vikuu kuanzisha programu za ukunga kwa wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita ili kuondoa ulazima wa kusoma stashahada ya uuguzi kabla ya kuanza shahada ya ukunga," amesema Dkt. Beatrice.




Ameongeza kuwa uuguzi na ukunga ni taaluma mbili tofauti, ingawa zinashirikiana kwa karibu, na kwamba si lazima mkunga kuwa muuguzi kwani kuna wakunga ambao si wauguzi lakini wanatenda kazi zao vizuri.




"Muundo wetu wa utumishi bado haimtambui mkunga kama taaluma inayojitegemea, tunaiomba serikali ifanye mabadiliko katika muundo wa utumishi ili kumtambua mkunga," amesisitiza Dkt. Beatrice.

Dkt. Beatrice ametoa wito kwa wakunga wenzake kuzingatia weledi na maadili katika utendaji wao na kuhakikisha wanapata mafunzo yanayoendana na mahitaji ya sasa.




Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya, Bi. Ziada Sellah, ameeleza kuwa bado kuna kazi kubwa ya kuwajengea uwezo wakunga, na mafunzo hayo yatawasaidia kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati.

Mafunzo hayo, yanayoendelea katika Mkoa wa Shinyanga, yamebeba kauli mbiu inayosema, "Thamini Uzazi Salama, Okoa Maisha ya Mama na Mtoto."








No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso