Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita akitoa mkono wa pole kwa mfiwa wa watoto wawili februari 18, 2025 katika kijijini Bulige, halmashauri ya Msalala wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.
NA NEEMA NKUMBI - HUHESO DIGITAL KAHAMA
Watu watano, wakiwemo watatu wa familia moja, wamefariki dunia baada ya kuzama katika dimbwi la maji lililopo kijijini Bulige, halmashauri ya Msalala wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.
Tukio hilo lilitokea Jumamosi, Februari 15, 2025, majira ya saa kumi jioni, ambapo watoto wawili walikuwa wakiogelea katika dimbwi hilo, ndipo walipoanza kuzama na Mwanamke mmoja alijaribu kuingia kwenye dimbwi hilo kwa lengo la kuwaokoa lakini naye alizama pia Watoto wawili wa mama huyo walijaribu kumsaidia nao walizama na kupoteza maisha.
Prisca Luchagula, mama wa watoto wawili waliopoteza maisha, amesema watoto wake walikuwa wametoka shambani na walipita eneo hilo na kuanza kuogelea ndipo watoto walizama na kufariki kwenye dimbwi hilo.
Mwenyekiti wa kijiji cha Bulige Allen Mahanga amesema dimbwi hilo limetokana na uchimbaji wa udongo (moramu) kwa ajili ya ujenzi wa makazi yao na wengine walichimba udongo wa mfinyanzi kwa ajili ya kufinyanga vitu mbalimbali.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Bulige, Emmanuel Mhina, amesema ndimbwi hilo linatumiwa na wananchi kuchota maji ya kufua na kuoga, jambo lililopelekea watoto kuingia na kuogelea pia dimbwi hilo liko sehemu iliyojificha, hivyo ni vigumu kuliona na kuliwekea uzio kama vile maeneo mengine ambayo yamewekewa uzio.
Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilayani Kahama, Stanley Luhwago, amethibitisha kupokea taarifa ya tukio hilo na amewataja waliokufa kuwa ni Zawadi Nkwambi (13), Khadija Nkwambi (11), Rahel Peter (11), Samike Peter (1), pamoja na mama mzazi wa Samike, Hoja Kubo (29).
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, ameyefika katika kijiji hicho Februari 18, 2025, kutoa pole kwa familia hizo, ambapo ametoa maelekezo kwa viongozi wa vijiji na vitongoji wilayani humo kuhakikisha wanachunguza maeneo yote yenye madimbwi au mabwawa ya maji na kuyalinda kwa kuwekewa uzio na milango ya kuingia na kutokea ili kuzuia maafa mengine yasitokee.
Pia Dc. Mboni amewataka Tarura na Tanroads kuwasimamia wakandarasi wanaotekeleza miradi, hususani ya barabara wilayani humo, kuhakikisha wanayafukia mashimo au kutengenezea uzio pindi wanapo amliza mazingira shughuli za uchimbaji wa udongo (moramu) kuepuka vifo visivyo vya lazima.
No comments:
Post a Comment