*Asema Falsafa ya 4R ya Rais Samia imesaidia kujenga jamii ya Watanzania yenye Amani, Umoja, Mshikamano.*
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali inatambua na kuthamini kazi inayofanywa na viongozi wa dini pamoja na wa kimila katika kuhakikisha nchi inakuwa na ustawi wa jamii.
Amesema ni jambo la faraja kuona wakati wote viongozi hao wamekuwa wakifanya kazi na kuvuka mipaka ya kiroho na kugusa ustawi na maendeleo ya jamii katika nyanja mbalimbali.
Ameyasema hayo leo Jumatano (Februari 26, 2025) alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Siku ya Maridhiano ( Maridhiano Day), iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Mkoani Arusha.
"Serikali inatambua na kuthamini mchango wenu mkubwa katika kufanikisha masuala muhimu ya kitaifa yanayowaunganisha Watanzania wote, ikiwemo uhamasishaji wa waumini katika kampeni mbalimbali muhimu kwa Taifa. Ninawasihi endeleeni kutoa ushirikiano huo kwani sauti zenu zina nguvu kubwa katika jamii."
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa viongozi hao kuendelea kushirikiana na Serikali katika kudumisha amani ili Watanzania waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali.
"Ninatambua JMAT iko kwa lengo hilo, hivyo endeleeni kuongeza wigo wa kuhamasisha na kudumisha upendo, amani umoja na mshikamano hapa nchini."
Amesema suala la kudhibiti mmomonyoko wa maadili limeendelea kuwa ajenda ya kudumu ya viongozi hao. "Ninawasihi sana endeleeni kukemea vikali vitendo vyote ambayo ni kinyume na maadili ya dini na utamaduni wa Mtanzania."
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema Falsafa ya 4R iliyoasisiwa na Rais Dkt. Samia imekuwa chachu katika kuimarisha Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Mabadiliko hivyo kujenga jamii ya Watanzania yenye Amani, Umoja, Mshikamano.
No comments:
Post a Comment