NA NEEMA NKUMBI - HUHESO DIGITAL KAHAMA
Mwanaume mmoja aitwaye John Julius, mkazi wa Mbika, Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama, alijeruhiwa vibaya na kupelekwa hospitalini baada ya kupigwa na sungusungu, kufuatia kudai ujira wa kulima shamba.
Tukio hili lilitokea Februari 15, 2025, baada ya John kwenda kwa mwajiri wake, Mwajuma Haroona kudai ujira wa shilingi 20,000, aliyotakiwa kupewa baada ya kumaliza kazi ya kilimo.
John ameeleza kuwa, baada ya kumaliza kazi, alikwenda kudai fedha zake, lakini Mwajuma alimuambia atangulie shambani ili akague shamba. Alipofika shambani, hakukutana na Mwajuma, alirudi tena nyumbani kwa mwajiri wake lakini alikataa kumlipa.
Hali hiyo ilimfanya John kusema, "nitachukua mlango badala ya hela yangu." Alipofika shambani kwa lengo la kuchukua mlango, alikuta ndugu wa Mwajuma ambaye alimtuhumu kuwa ni mwizi, sungusungu walimkamata na kumshambulia John kabla ya kumpeleka kwa Mwajuma ambaye alikiri kuwa alikuwa anamdai.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mbika, Benedicto Mangane, amethibitisha kuwa watuhumiwa walikamatwa na kupelekwa polisi, huku John akipelekwa hospitali kwa matibabu.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Ushetu, Richard William, amethibitisha kumpokea mgonjwa huyo akiwa na majeraha na kuanza matibabu ya awali, Baada ya uchunguzi wa awali ilibainika kuwa amevunjika mguu na anatarajiwa kupatiwa rufaa kwa uchunguzi zaidi.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga SACP Janeth Magomi amethibitisha tukio hilo na kuwataja wanaoshikiliwa kwa tuhuma hizo kuwa ni Bundala Dalali na Issack Kulwa ambao ni walinzi wa jadi(sungusungu) na kwamba upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea na utakapo kamilika watafikishwa mahakamani.
"Tunawashikilia Watuhumiwa wawili ambao ni Bundala Dalali na Issack Kulwa kwa kuhusika na tukio hili na upelelezi unaendelea tukikamilisha tutawafikisha Mahakamani,niwaombe Wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na kama mtu amekamatwa kwa tuhuma ya wizi ni bora akafikishwa polisi,"amesema Magomi.
No comments:
Post a Comment