Mkuu wa mkoa Anamringi Macha akizungumza na wadau wa elimu leo februari 24,2025 katika kikao kazi cha tathimni ya elimu Mkoani shinyanga.
NA NEEMA NKUMBI-HUHESO DIGITAL KAHAMA
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, amewataka walimu kuepuka mikopo umiza inayosababisha msongo wa mawazo, hali inayochangia kushindwa kwao kutekeleza majukumu yao ya ufundishaji kwa ufanisi.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao kazi cha tathmini ya hali ya elimu Mkoa wa Shinyanga, kilichofanyika leo, februari 24, 2025 katika Manispaa ya Kahama RC Macha amesema kuwa walimu wanatakiwa kubadilika kuendana na teknolojia ili kukidhi mahitaji ya dunia, ambapo pia amehimiza walimu kufanya kazi kwa juhudi ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
"Tunatakiwa kuweka nguvu katika elimu ili kuendelea kubadilika kulingana na ushindani wa dunia, aneyefanya kazi vizuri ananifanya nisifoke foke kwani hasira hupunguza maisha," amesema Mkuu wa Mkoa.
RC Macha pia amesisitiza matumizi sahihi ya teknolojia, akieleza kwamba teknolojia ikiwa inatumika ipasavyo, itasaidia wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao,pia ameongeza kuwa tathmini ya miaka mitano inayoonyesha Mkoa wa Shinyanga haujafanya vizuri changamoto inayohitaji kujitathmini.
Pia amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya ya Kahama kuhakikisha kuwa wanafunzi wanakaa katika madawati ili kutekeleza agizo la Serikali.
Aidha, amewashukuru wakurugenzi wa shule binafsi kwa juhudi zao katika kuongeza ufaulu wa wanafunzi, akisema kuwa hilo pia linasaidia Serikali kupunguza gharama za uendeshaji wa baadhi ya wanafunzi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, akitoa salamu za Wilaya, amesisitiza kuwa ili azma ya Rais Samia Suluhu Hassan kutimiza malengo yake, ni muhimu maeneo ya shule yanayojengwa yaweze kufikika kwa urahisi, na chakula mashuleni kiwekwe mbele.
Baadhi ya wadau wa elimu walio hudhuria kikao hicho wametoa maoni yao,
Anderson Lyimo amesema wazazi wanachangia katika kufeli kwa wanafunzi kwani hawakagui watoto wao kuwa wamefika shuleni na kujua maendeleo ya watoto wao.
Mabula Magunila amesema ufaulu wa wanafunzi unashuka kutokana na baadhi ya shule kukosa walimu wa masomo husika hali inayopelekea wanafunzi kusoma wakati wa likizo na wakifungua shule hawasomi tena masomo hayo.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Thomas Muyonga amempongeza Mkuu wa Mkoa Rc Macha jinsi anavyoshirikiana na wadau wa elimu ili kutekeleza ilani ya chama, pia amewataka walimu kuzifanyia kazi changamoto zilizosemwa.
No comments:
Post a Comment