DC MBONI AONGOZA ZOEZI LA KUAGA MIILI YA WACHIMBAJI WALIOKUFA KATIKA MGODI WA NKANDI KAHAMA. - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday, 5 February 2025

DC MBONI AONGOZA ZOEZI LA KUAGA MIILI YA WACHIMBAJI WALIOKUFA KATIKA MGODI WA NKANDI KAHAMA.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, akitoa hotuba ya faraja na wito wa tahadhari kwa wachimbaji wengine.
Miili ya marehemu waliokufa katika ajali katika mgodi wa Nkandi Kahama
 Penina Nyagwaswa, ndugu wa marehemu, akizungumza mbele ya waandishi wa habari wakati wa zoezi la kuaga miili ya wachimbaji.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, akitoa hotuba ya faraja na wito wa tahadhari kwa wachimbaji wengine.




NA NEEMA NKUMBI - HUHESO DIGITAL KAHAMA

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mkoani Shinyanga, Mboni Mhita, ameongoza zoezi la kuaga miili ya wachimbaji wadogo wawili kati ya watatu waliofukiwa na kifusi katika mgodi wa Nkandi, ulio katika Kata ya Zongomela, Manispaa ya Kahama.


Akizungumza baada ya zoezi hilo, Mboni ametoa wito kwa wachimbaji wa mgodi huo na mingine kuendelea kuchukua tahadhari, hasa katika kipindi cha mvua nyingi zinazoendelea kunyesha.

"Sote tunafahamu kuwa mazingira ya ajali hii kutokea ilikuwa ni katika kutafta riziki, serikali iko pamoja na ninyi na imekuwa pamoja nanyi tangu siku ya kwanza ya tukio hilo, na niwaombe wachimbaji kuendelea kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua," amesema Mboni.


Ndugu wa marehemu, Penina Nyagwaswa, ameeleza kuwa tukio hili limetokea kwa mapenzi ya Mungu na akashukuru serikali kwa ushirikiano katika kipindi hiki cha majonzi.

"Tunashukuru kwa kila jambo maana hilo limetokea ni kwa mapenzi ya Mungu. Napenda kuishukuru Serikali kwa kuwa pamoja na sisi hadi leo, tunakwenda Meatu kwa ajili ya maziko. Pia nashukuru uongozi wa mgodi kwa kushirikiana na sisi katika hatua zote hadi sasa," amesisitiza.


Meneja wa mgodi huo, Mdaki Shabani, amethibitisha kuwa jitihada za kuokoa mwili wa tatu zinaendelea, ingawa amelalamikia ukosefu wa umeme kama changamoto kubwa.

"Jitihada za kuutafuta mwili mwingine uliosalia zinaendelea japo changamoto kubwa ni umeme, kwani pampu tulizofunga zinashindwa kuvuta maji kutokana na ukosefu wa umeme. Niombe wenzetu wa TANESCO kuliangalia jambo hili, kwani kama mgodi tunahitaji nishati hiyo kuliko kitu kingine katika wakati huu ili kufanikisha jitihada za maokozi," amesema Shabani.


Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO Wilaya ya Kahama, Kisika Eliya Kisika, amethibitisha kupitia simu kwamba hakuwa na taarifa ya kukosekana kwa umeme katika mgodi huo.


Baada ya zoezi la kuaga miili, miili hiyo imesafirishwa kuelekea Meatu, Mkoani Simiyu kwa ajili ya maziko.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso