Afisa mtendaji Kata ya Zongomela Emmanuel Mrosso akizungumza na wanachama wa Ccm Mtaa wa Ilindi katika maadhimisho ya miaka 48 ya Ccm.
NA NEEMA NKUMBI - HUHESO DIGITAL KAHAMA
Changamoto ya miundo mbinu ya barabara inayounganisha Mtaa wa Ilindi, Kata ya Zongomela Manispaa ya Kahama na ofisi za Kata hiyo inaenda kutatuliwa, Afisa Mtendaji wa Kata ya Zongomela, Emmanuel Mrosso, amesema kuwa watajenga karavati la muda huku wakisubiri TANROADS Shinyanga kumaliza ujenzi wa karavati la kudumu.
Katika maazimisho ya miaka 48 ya Chama cha Mapinduzi (CCM) yaliyofanyika Mtaa wa Ilindi, Mrosso ameeleza kuwa mwaka jana walifungua barabara kupitia fedha za halmashauri, na mwaka huu wanatarajia kutengeneza mitaro na kuweka makaravati katika maeneo yanayoshindwa kupitika.
"Tumeshawasiliana na TANROADS Shinyanga, na wameshajibu. Wakati tunasubiri bajeti kwa ajili ya karavati la kudumu, tutajenga kivuko cha muda kusaidia wakazi wa Ilindi," amesema Mrosso.
Sambamba na hilo, wananchi wa Mtaa wa Ilindi wamepanda miti katika Shule ya Msingi Kidete kama sehemu ya sherehe za miaka 48 ya CCM, Mrosso amewataka wananchi kushirikiana na walimu kutunza miti hiyo, kwani itasaidia kwa matunda, kivuli, na mbao itakapotunzwa vizuri.
Mwenyekiti wa CCM Mtaa wa Ilindi, Bi. Fatuma Hussein, amesema kuwa wamepanda miti mia tano katika shule hiyo wametembelea watoto yatima katika Kituo cha New Hope kilichopo Mtaa wa Ilindi.
Wanachama wa CCM walitoa msaada kwa watoto yatima kama sehemu ya maadhimisho hayo ambapo Martha Matanga, mmoja wa wanachama, amesema miti imepandwa kwa ajili ya Kijani cha Rais Samia, na kwamba shule hiyo haikuwa na miti ya kivuli.
Pia Steven Peter, mwanachama mwingine aliyehudhuria, amesema msaada kwa watoto yatima umelenga kuwaonyesha upendo na kuwapa moyo, kwani watoto hao hawakutaka kuwa yatima.
No comments:
Post a Comment