Menejimenti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imekutana na Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi na kuwasilisha mapendekezo ya maboresho yanayoigusa moja kwa moja Wizara ya Mambo ya Nje na wadau wake katika kikao kazi kilichofanyika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo ameeleza kuwa Wizara yake ndiyo kiungo muhimu kati ya wawekezaji wa nje na sekta za Tanzania na hivyo zipo changamoto za kikodi zilizowasilishwa mezani kwake ambazo kutatuliwa kwake kutaongeza ushindani wa kiuchumi Tanzania.
Ameongeza kuwa ipo haja ya kuimarisha mifumo ya ulipaji kodi kidijitali na kuifanya iwe rafiki kwa walipa kodi waliopo ndani na nje ya nchi; lakini pia mifumo ya uombaji viza kuwa rafiki ili kuvutia watalii na wawekezaji kuja kwa wingi nchini, huku akitolea mfano akiwa Balozi wa Italia kwa mwaka waliweza kuzalisha mapato yatokanayo na viza ya $10M sawa na bilioni 24.8 za Kitanzania.
“Mtu anaamua kuahirisha safari yake au kwenda nchi nyingine kutokana na changamoto za kimfumo, jambo ambalo linaifanya nchi kupoteza mapato yanayotokana na visa ” amesisitiza.
Kwa upande wake Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel M. Tutuba ameeleza umuhimu ya utoaji elimu ya mlipa kodi kuwa endelevu,ili kuwezesha mifumo mbalimbali ya kulipa kodi kuweza kusomana lakini pia walipaji wazuri wa kodi kupewa tuzo zenye kuthamini mchango wao katika ujenzi wa Taifa.
Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mhe. Balozi Ombeni Sefue ambaye alianza kwa kuwataka watoa mapendekezo kuwa wawazi kabisa ili kusaidia kujenga mfumo ulio bora wa ulipaji kodi.
No comments:
Post a Comment