USHETU
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha leo tarehe 29 Januari, 2025 amefanya ziara na kutembelea Vijiji vya Nsunga, Manungu na Bugoshi vilivyopo Kata ya Uyogo Halmashauri ya Ushetu na kuzungumza na wakulima wa zao la Pamba ili kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo.
RC Macha amesema kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha inashirikiana vyema na wakulima pamoja na Vyama vya Kilimo na Masoko (AMCOS) ili kuwasaidia wakulima waongeze uzalishaji wa zao la pamba kwa angalau wazalishe kuanzia kilo 1200 au zaidi na hivyo kukuza uchumia wao na pato la Mkoa kwa ujumla.
“Niwapongeze kwa juhudi zenu za uzalishaji wa zao hili la pamba, lakini niwahakikishie kwamba Serikali iko pamoja nanyi bega kwa bega kuhakikisha kwamba tunainua na kuongeza kiwango cha uzalishaji ili angalau kila mmoja wetu azalishe kuanzia kilo 1200 za pamba, na kwa kufanya hivyo kutakuza uchumi wa familia zetu pamoja na Mkoa wetu,” amesema RC Macha.
RC Macha akiwa ameambatana na Mhe. Mboni Mhita ambaye ni DC wa Kahama amewaasa wakulima walime pamba kwa kuzingatia utaalamu na watumie viuatilifu ili pamba wanayovuna iwe bora na iendane na kiwango walicholima kwani Serikali inajitahidi pia kutafuta bei nzuri ya pamba wanayozalisha kadiri iwezekanavyo na kuona kwamba zao hili linarudisha heshima na thamani yake kama ilivyokuwa awali.
Pia amewasisitiza Maafisa Ugani wa Halmashauri ya Ushetu kuendelea kushirikiana vizuri na wakulima pamoja na kufanya ufuatiliaji na mwenendo wa uzalishaji wa zao hilo pamoja na kuhakikisha dawa za kuulia wadudu, bomba za kupulizia wadudu pamoja na mbegu za pamba zinapatikana kwa wakati na kugawiwa kwa usawa ili wakulima wazalishe kwa tija.
Kando na hayo, ameendelea kuwakumbusha pale wanapopata faida baada ya kuuza pamba waweze kutunza kiwango fulani cha pesa kwa ajiri ya kilimo cha msimu unaofuata pamoja na kutumia vizuri pesa kuboresha maisha ya familia zao.
Kwa ujumla, kata ya Uyogo ina idadi ya wakulima wa pamba takribani 799, hekari zilizolimwa mpaka sasa ni takribani 2003, pia mbegu zilizopokelewa ni zaidi ya Tani 33 huku pampu za kunyunyuzia wadudu pamoja na mbegu zimegawiwa.
No comments:
Post a Comment