Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga SACP Janeth Magomi
NA NEEMA NKUMBI - HUHESO DIGITAL SHINYANGA
Mzee Joseph Tuju, mwenye umri wa miaka 73, amefariki dunia kwa kujinyonga katika nyumba yake mtaa wa Azimio, kata ya Lubaga, Manispaa ya Shinyanga.
Tukio hilo lilitokea Januari 6, 2025 ambapo Diwani wa kata ya Chibe, Mhe. Kisandu John, amesema alipewa taarifa na majirani, ambao waliona nzi wengi kwenye dirisha la nyumba ya marehemu, jambo lililowalazimu kuwahi kutoa taarifa kwa familia na polisi na Polisi waligundua mwili wa marehemu ukiwa umejinyonga kwa kutumia shuka.
Familia ya marehemu inasema kuwa kifo hiki si cha kwanza, kwani Mzee Joseph anakuwa mtu wa nne kufariki kwa kujinyonga katika familia yao, wakiwemo mama yao, kijana mmoja kutoka Kahama, na binti mwingine.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, amethibitisha tukio hili na kusema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha kifo hicho ni msongo wa mawazo kutokana na maradhi aliyokuwa akiyapata marehemu kwa muda mrefu.
Kamanda Magomi amekemea vitendo vya kujinyonga, akisisitiza kuwa si suluhisho la changamoto za maisha na kusema kuwa jamii inapaswa kuepuka hali hii, Mazishi ya Mzee Joseph yamefanyika leo katika mtaa wa Azimio.
No comments:
Post a Comment