Na Waandishi wetu,
Maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa wananchi walio na sifa ya kujiandikisha katika mikoa ya Njombe, Rukwa na sehemu ya Mkoa wa Ruvuma kwenye Halmashauri za Wilaya ya Nyasa, Mbinga, Mbinga Mji, Wilaya ya Songea na Manispaa ya Songea imepamba moto kwa kuanza kwa mafunzo kwa watendaji wa uboreshaji wa Daftari katika ngazi ya mkoa katika mikoa hiyo minne.
Mafunzo hayo yamefunguliwa leo tarehe 01 Januari, 2025 na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mhe. Jaji Jacobs Mwambegele kupitia hotuba yake ambayo imesomwa na wawakilishi wake katika Mikoa ya Songwe, Rukwa, Njombe na Ruvuma.
Katika hotuba yake, Jaji Mwambegele amewataka watendaji hao kuhakikisha kuwa wanatunza vifaa vya uandikishaji ili viweze kutumika na wananchi katika maeneo mengine nchini ambayo bado hawajapata fursa ya kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Amewasisitiza Watendaji hao ambao ni Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa halmashauri kuwa kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa hivi kutapelekea athari kubwa katika ukamilishaji wa zoezi hili muhimu.
Kwa kusisitiza, ni muhimu kutekeleza majukumu yenu kwa umakini katika kila eneo ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uandikishaji hasa ikizingatiwa kuwa, vifaa hivi vimenunuliwa kwa gharama kubwa sana na vinatarajiwa kutumika katika maeneo mengine ya uandikishaji nchini, amesema Jaji Mwambegele.
Akizungumzia kuhusu Mafunzo hayo, Jaji Mwambegele ameeleza kuwa yanahusisha namna ya ujazaji wa fomu pamoja na kutumia mfumo wa kuandikisha wapiga kura (Voters Registration System - VRS) ili waweze kupata uelewa wa pamoja utakaowapa fursa ya kutumia kwa ufasaha mfumo huo pamoja na vifaa vingine vya kuandikisha wapiga kura.
Mafunzo haya, yanawajengea umahiri wa kuwafundisha Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata kisha nao watatoa mafunzo hayo kwa Waendeshaji wa Vifaa vya Bayometriki na Waandishi Wasaidizi ambao ndio watahusika na uandikishaji wa wapiga kura vituoni, amesema Jaji Mwambegele.
Aidha, Maafisa TEHAMA watapatiwa mafunzo maalum ya jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiufundi (Troubleshooting) endapo zitajitokeza wakati wa zoezi la uandikishaji wa wapiga kura vituoni.
Mapema kabla ya kuanza mafunzo hayo, washiriki wamesimama kwa dakika moja kwa ajili ya kumkumbuka aliyekuwa Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mheshimiwa Mwanaisha Kwariko ambaye amefariki hivi karibuni nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.
No comments:
Post a Comment