Na. Paul Kasembo, KISHAPU.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewataka watumishi wa Kituo cha Huduma Jumuishi (One Stop Centre) kilichopo hapa Kishapu kutunza siri za manusura na wahanga wa ukatili wa kijinsia wanaokuja kutoa taatifa na kupatiwa huduma katika kituo hiki huku akitoa wito kwa wananchi wa Kishapu kukitumia vema na kikamilifu kwani lengo ni kutokomeza kabisa vitendo hivi visivyofaa.
RC Macha ameyasema haya leo tarehe 16 Desemba, 2024 wakati akizindua kituo hiki ambacho kimejengwa kwa ufadhili wa Nchi ya Finland kupitia Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi Duniani (UNFPA) ambapo pamoja na kazi nyingine lakini kituo kitatoa huduma kamili za matibabu, kisheria na ushauri wa kisaikolojia kwa manusura na wahanga wa ukatili wa kijinsia na watoto wao katika sehemu moja. Huduma hizi zinaweza pia kupatikana kupitia mifumo rasmi au isiyo rasmi.
"Niwatake ninyi watumishi wa kituo hiki kuhakikisha kuwa mnatunza siri zote za manusura na wahanga wa vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia wanaokuja hapa kupatiwa huduma zenu, na hili agizo ni kukazia sehemu ya viapo na maadili yenu ya kitaaluma," amesema RC Macha.
Kwa upande wake Mark Bryan Schreiner ambaye ni Mwakilishi Mkaazi wa UNFPA Tanzania amesema kuwa Shirika lao litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha kuwa kunatokomezwa kabisa kwa mambo yote yanayohusu ukatili wa kijinsia na kuyalinda makundi maalum yakiwemo ya wanawake na watoto katika Mkoa wa Shinyanga na Tanzania kwa ujumla.
Aidha Mr Juhana Lehtinen ambaye ni Mkuu wa Ushirikiano Ubalozi wa Finland Tanzania amempongeza RC Macha kwa utendaji kazi wake huku akiishukuru zaidi Serikali ya Tanzania kwa kuendelea na mikakati ya utokomezaji wa ukatili wa kijinsia kwa wananchi wake na kupongeza kwa kazi nzuri inayofanywa na Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Mkoa wa Shinyanga (SHIVYWATA) kwa kuendelea kuwaunganisha walengwa wote.
Kwa ujumla, Ukatili wa Kijinsia unatajwa kuwa ni pamoja na kitendo kinachofanywa dhidi ya mtu kwa sababu ya jinsia yake. Wanaume na wanawake wanaweza kupitia ukatili wa kijinsia, lakini manusura na wahanga wengi zaidi ni wanawake, wasichana na watoto ambapo kuanzia Machi 2024 hadi Desemba 2024 kumeripotiwa takribani vitendo 192 katika Kituo hiki cha Kishapu pekee.
No comments:
Post a Comment