Na. Paul Kasembo, Kishapu,
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Mkude amewaasa wananchi wa Kata ya Shagihilu na Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla kushirikiana na vyombo vya dola kuripoti taarifa sahihi na haraka wanapoona matukio ya ukatili wa kijinsia yakitokea katika maeneo wanayoishi ili kuhakikisha wanapunguza na kutokomeza ukatili unaofanyika na kuifanya jamii ibaki salama.
DC Mkude ametoa wito huu leo tarehe 10 Desemba, 2024 wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia mkoani Shinyanga akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha, maadhimisho ambayo yamefanyika katika Shule ya Msingi Shagihilu iliyopo Kata ya Shagihilu Wilaya ya Kishapu yakiwa na Kauli Mbiu isemayo “Kuelekea Miaka 30+ ya Beijing: Chagua Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia”.
“Serikali inaendelea na jitihada za kutokomeza ukatili wa kijinsia katika Mkoa wetu lakini ombi langu kwenu wananchi ni kwamba muwe tayari kushirikiana na vyombo vya dola kwa kuripoti na kutoa taarifa sahihi haraka mnapoona au kusikia matukio ya ukatili yanafanyika katika maeneo yenu kwani lengo letu sote ni moja kuhakikisha tunakomesha kabisa matukio haya na kuifanya jamii yetu iwe sehemu salama zaidi” amesema DC Mkude
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Shinyanga Bi. Lidya Kwesigabo akiwasilisha taarifa juu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa Mkoa wa Miaka Mitano wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto amesema kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na Taasisi na Mashirika yasiyo ya Kiserikali wameshiriki na kuhamasisha utoaji wa elimu ya ukatili dhidi ya watoto mashuleni, kutoa huduma ya msaada wa kisheria pamoja na kuunda madawati ya ulinzi wa mtoto ili kuzuia matukio ya ukatili wa kijinsia katika jamii.
Kwa mujibu wa Utafiti wa Maendeleo ya Watu na Afya Tanzania (TDHS) kwa mwaka 2022 matukio ya ukatili wa kijinsia mkoani Shinyanga yalipungua na kufikia asilimia 28 ukilinganisha na mwaka 2010 ambapo ilikuwa ni asilimia 34, lakini pamoja na yote jitihada zinaendelea kufanyika kuhakikisha matukio haya yanapungua kwa kuleta huduma za kijamii zikiwemo elimu, afya, maji pamoja na miundombinu ili kuwaweka wananchi sehemu salama kutokana na ukatili wa kijinsia.
No comments:
Post a Comment