Na. Paul Kasembo, SHINYANGA DC.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha, amewataka Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji waliochaguliwa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27, 2024 kwenda kuwa suluhisho na siyo kuwa vyanzo au sehemu ya migogoro ya wananchi ikiwemo migogoro ya ardhi huku akisisitiza kuziishi R nne za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwatumikia wananchi wao.
RC Macha ameyasema haya leo tarehe 18 Desemba, 2024 alipokuwa akifungua Mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi takribani 982 wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Shule ya Sekondari Shinyanga Wasichana ambapo pamoja na mambo mengine amewakumbusha kufanya kazi kwa kuzingatia uadilifu, uzalendo, kudumisha amani, kufanya kazi kwa kuzingati sheria, kanuni na taratibu za nchi na kusimamia vyanzo vya mapato.
Pia wamekumbushwa kwenda kufanya kazi kwa ushirikiano na viongozi wa dini, kutoa huduma bila kujali itikadi za vyama, kusoma mapato na matumizi, kuepuka rushwa, kutowatoza gharama yoyote ili kupata huduma wananchi, kuepuka ulevi, kuzuia ukatili wa kijinsia, kusimamia miradi ya maendeleo, kuhamasisha utunzaji wa mazingira na upandaji wa miti katika maeneo yote ya makazi na wazi.
Wamesisitizwa pia kwenda kutoa hamasa kwa wananchi kujiunga na Bima ya afya, kuhamasisha wananchi kutumia vyandarua kwa usahihi na kufuatilia na kuhakikisha watoto wote wanaostahili kuanza masomo Januari 2025 wanapelekwa shule na kwa msisitizo zaidi wote wenye ulemavu wasiachwe majumbani kwa namna yoyote ile.
"Pamoja na pongezi kwenu kwa kuchaguliwa na kuaminiwa na wananchi, niwatake kwenda kuwa suluhisho na tiba na siyo kuwa vyanzo au sehemu ya migogoro kwa wananchi wetu hasa migogoro ya ardhi, zingatieni sana R nne za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uhudumu wenu kwa wananchi," amesema RC Macha.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi hawa wamemuahidi RC Macha kuwa yale yote aliyoshauri, kuelekeza na kusisitiza wameyapokea na watakwenda kuyafanyia kazi ili kuleta ustawi, amani na kuwa sehemu ya mabadiliko kwa wananchi wao.
Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya RC Macha aliyoyatoa tarehe 29 Novemba, 2024 wakati wakiapishwa ambapo aliwataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuwapatia mafunzo kabla ya Desemba 2024.
No comments:
Post a Comment