Na Paul Kaanda, Mbogwe.
MRADI mkubwa wa ujenzi wa barabara ya Igalula, inayounganisha kata ya Ilolangulu na Nanda katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, mkoani Geita, unaendelea vizuri.
Barabara hiyo, ambayo ni muhimu sana kwa maslahi mapana ya wananchi Jimbo la Mbogwe na Wilaya kwa ujumla ambapo kwa muda mrefu ilikuwa ni kilio kikubwa kwao.
Hata hivyo, kupitia Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, Nicodemus Maganga, wananchi sasa wanashuhudia utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu hiyo ya barabara.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari, wananchi wa maeneo hayo wameeleza furaha yao kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Mbunge wao na Serikali kwa ujumla, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wananchi wamesema kuwa wanashukuru kuona Serikali ikiwajali na kutatua changamoto za miundombinu.
Baraka Steven, mmoja wa wakazi wa kata hizo, amesema: "Ilikuwa ni changamoto kubwa sana huko nyuma, lakini kwa sasa tunaishukuru sana Serikali na Mbunge wetu Maganga, anafanya kazi kubwa mno ya kuwatumikia wananchi. Tunaendelea kumuombea kwa Mungu yeye pamoja na Mheshimiwa Rais ili waendelee kutimiza ahadi zao kwa wananchi."
Baraka ameongeza: "Ndugu zangu wandishi, kama mnavyojua sisi ni wakulima, hivyo ujenzi wa barabara hizi unakwenda kurahisisha usafirishaji wa mazao yetu, na pia kuunganisha kata hadi kata."
Wananchi hao wameeleza kuwa, licha ya ujenzi wa barabara, wanashuhudia pia maendeleo katika maeneo mengine, kama vile miundombinu ya umeme, ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, visima vya maji, na miradi mingine mbalimbali ambayo imekuwa na manufaa makubwa kwao.
Hadi sasa Juhudi hizi za ujenzi wa miundombinu zinaonekana kuwa na athari chanya kwa maisha ya wananchi wa Mbogwe.
No comments:
Post a Comment