WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuendelea kutatua changamoto za walimu zikiwemo za malimbikizo ya madeni na upandishaji wa madaraja.
Amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua, anathamini na kuheshimu kazi kubwa inayofanywa na walimu wote nchini katika kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kukuza na kuiendeleza sekta ya elimu nchini.
Amesema hayo leo (Alhamisi, Desemba 12, 2024) alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 19 wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari (TAHOSSA) uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Jakaya Kikwete jijini Dodoma
“Kwa sasa suala la stahiki za walimu linaendelea kuzingatiwa na Serikali imeendelea kufanya jitihada kubwa za kuhakikisha inapadisha madaraja watumishi walimu waliokosa na wanaopaswa kupandishwa, Serikali imedhamiria kuondoa msamiati wa areas (malimbikizo ya mishahara).”
Amesema kuwa katika kipindi cha (mwaka 2021/2022 hadi mwaka 2023/2024), Serikali imepandisha madaraja ya walimu 227,383 na kuwabadilishia miundo walimu 20,436.“ Ofisi ya Rais-TAMISEMI hakikisheni kila anaepanda daraja analipwa stahiki zake kwa wakati.”
Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa katika kipindi cha 2021/22 hadi 2023/24, jumla ya shilingi trilioni 1.76 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya shule ikiwemo ukarabati na ujenzi mpya.
“Miundombinu hii imesaidia kwa kiasi kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda shuleni.”
Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa Sera ya Elimu bila Malipo, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali imeendelea kutoa shilingi bilioni 33.3 kwa mwezi kwa ajili ya shule zote za Msingi na Sekondari za Serikali nchini ikiwa ni za uendeshaji wa shule pamoja na posho za madaraka.
“Wakati tunaanza mpango huu mwaka 2015/16 kila mwezi ilikuwa inatolewa shilingi bilioni 13.46, hivyo ongezeko hili ni sawa na asilimia 147.26. Utaratibu huu umekuwa chachu ya kuimarisha uandikishaji na mahudhurio ya wanafunzi katika ngazi mbalimbali.”
No comments:
Post a Comment