RPC JANETH MAGOMI AMEZINDUA KITUO CHA POLISI MHONGOLO MANISPAA YA KAHAMA. - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday, 18 December 2024

RPC JANETH MAGOMI AMEZINDUA KITUO CHA POLISI MHONGOLO MANISPAA YA KAHAMA.


Mkuu wa Polisi Mkoa wa Shinyanga (RPC), Janeth Magomi, akizungumza na wananchi mara baada ya uzinduzi rasmi wa kituo cha Polisi Mhongolo.



NA NEEMA NKUMBI- HUHESO DIGITAL KAHAMA


Mkuu wa Polisi Mkoa wa Shinyanga (RPC), Janeth Magomi, amezindua rasmi kituo kipya cha polisi cha Mhongolo, kilichopo Manispaa ya Kahama, kwa lengo la kuimarisha usalama na huduma za polisi kwa wananchi wa maeneo hayo.


Uzinduzi huo umefanyika leo, Desemba 18, 2024, katika sherehe iliyohudhuriwa na viongozi wa serikali, maafisa wa polisi, na wananchi wa Kahama, RPC Janeth Magomi ameeleza kuwa uwepo wa kituo hicho ni hatua muhimu katika kupambana na uhalifu na kuboresha usalama katika Manispaa ya Kahama na maeneo jirani.


Akizungumza wakati wa uzinduzi, RPC Magomi amesema: "Jeshi la Polisi, tushukeni sasa kwa wananchi, tukatende kazi kwa ueledi na tuhakikishe tunafanya kazi kwa pamoja, Mimi naahidi kuwa mlezi wa kituo hiki na kitakuwa na huduma muhimu za kiusalama, ikiwemo kufungua kesi, doria za kila siku, na msaada kwa wahanga wa uhalifu, Pia, tutahakikisha uwepo wa maafisa wa polisi ili kudhibiti matukio ya uhalifu katika eneo hili."


Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kahama, Mtaju Mayombo, amesema kuwa kituo hicho kitachangia pakubwa katika kupunguza matukio ya uhalifu, hususani wizi, uvunjaji wa amani, na makosa ya barabarani. "Tutahakikisha kuwa ufanisi wa kazi yetu unakuwa mkubwa kwa kushirikiana na wananchi ili kutimiza malengo yetu ya kulinda usalama. Hatutawapa mwanya wa kufanya uhalifu," amesema Kamanda Mayombo.


Aidha, Mwanasheria Stephen Magalla, ambaye amemwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, ameeleza kuwa katika bajeti ya mwaka 2024/2025, wametenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo viwili vya polisi katika kata za Nyasubi na Zongomela, kwa kutambua umuhimu wa jeshi la polisi katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.


Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Mhongolo, Magembe Chimu, amesema kuwa wafanyabiashara wa Mhongolo walijikusanya ili kusaidia upatikanaji wa kituo hicho, baada ya kushuhudia wizi na uhalifu mwingi ambao ulileta usumbufu mkubwa katika shughuli zao za biashara.


Mwananchi mmoja wa Mhongolo, Sharifu Said, amesema kuwa wamefurahi kupata kituo hicho cha polisi kwani uhalifu ulikuwa umekithiri katika eneo hilo. "Tulikuwa tukihofia kupoteza biashara zetu na wengi walikuwa wakifunga mapema kutokana na hofu ya kuibiwa," amesema Sharifu.


Mwananchi mwingine, Rhoda Shigela, amesema kuwa uanzishwaji wa kituo hicho utasaidia kupunguza hofu ya uhalifu na kuongeza ushirikiano kati ya polisi na jamii. "Kituo hiki kitatufaa sana, hasa kwa wanawake, kwani tutakuwa na mahali pa kutoa taarifa za matukio ya unyanyasaji, na hivyo kupunguza uhalifu," amesema Rhoda.


Awali akisoma taarifa ya ufunguzi wa kituo hicho , Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Mhongolo, Anitha Ngeiyamu, amesema kuwa wazo la kuanzisha kituo kidogo cha polisi lilianza baada ya matukio mbalimbali ya kihalifu katika kata hiyo. "Tulishirikiana na wadau mbalimbali, wananchi, na ofisi ya OCD Kahama ili kuhakikisha tunapata suluhisho la kudumu la usalama."


Kituo cha polisi cha Mhongolo kimelipiwa kodi ya pango la mwaka mzima kwa msaada wa wafanyabiashara, wananchi, na ofisi ya OCD Kahama, Kituo hiki kitaimarisha ulinzi na usalama kwa wakazi zaidi ya 45,000 wa kata ya Mhongolo, kulingana na sensa ya mwaka 2022.
Wananchi wa Mhongolo wakiwa katika kituo cha polisi Mhongolo kushuhudia uzinduzi wa kituo hicho
Mkuu wa Polisi Mkoa wa Shinyanga (RPC), Janeth Magomi, akizungumza na wananchi mara baada ya uzinduzi rasmi wa kituo cha Polisi Mhongolo.

RPC Janeth Magomi akiwa mbele ya jengo jipya la kituo cha polisi cha Mhongolo, akifanya zoezi la uzinduzi rasmi kwa kukata utepe.
Mkuu wa Polisi Mkoa wa Shinyanga (RPC), Janeth Magomi, akizungumza na wananchi mara baada ya uzinduzi rasmi wa kituo cha Polisi Mhongolo.




No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso