Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Mkude
Na Mapuli Kitina Misalaba
Watoto wawili wamefariki dunia baada ya kushambuliwa na mnyama aina ya fisi katika Kata ya Igaga, Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga, huku watu wengine sita wakijeruhiwa.
Misalaba Media imezungumza na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Joseph Mkude, ambaye amethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa fisi huyo alitokea katika maeneo ya hifadhi ya milima ya Mawa na kuingia katika makazi ya watu mnamo Desemba 12, 2024, majira ya saa tano hadi saa saba mchana.
Kwa mujibu wa maelezo yake, fisi huyo aliendelea kuvamia makazi ya watu ambapo alimjeruhi mama mmoja na kisha kuingia ndani ya nyumba na kuwaua watoto wawili, Mussa Philip (miaka nane) na Stephano Philip (miezi minane), ambao ni wa familia moja.
“Fisi huyo alionekana ghafla majira ya saa tano hadi saa saba mchana, akitokea maeneo ya hifadhi ya milima ya Mawa. Hadi sasa bado hatujafahamu kwa nini alitoka kule na kuja maeneo ya wananchi nyakati hizi.”
“Baada ya kufuatilia, tumegundua kuwa fisi huyo alikuwa amejeruhiwa. Kila alipokutana na mtu, alimshambulia. Alianza kumshambulia mtoto wa kike aliyekuwa akichunga ng’ombe karibu na nyumbani. Binti huyo alipiga kelele, na mzee mmoja alijaribu kumuokoa, lakini naye akajeruhiwa.”
“Fisi huyo aliendelea hadi kwenye makazi ya watu kijijini kabisa. Alimvamia mama mmoja mwenye watoto wawili. Watoto hao walikuwa ndani ya nyumba, na mama huyo alipokuwa akijaribu kumzuia fisi, naye alijeruhiwa. Baadaye, fisi huyo aliingia ndani ya nyumba na kuwashambulia watoto hao wawili, hali iliyosababisha vifo vyao.”amesema DC Mkude
Jeshi la wanyamapori lilifika eneo la tukio haraka mara baada ya taarifa kutolewa, lakini fisi huyo alishauawa na wananchi kabla ya askari kufika.
“Sasa, hatua tulizochukua ni pamoja na kuwaita askari wa wanyamapori, ambapo watatu walifika mapema. Pia, maafisa wa wanyamapori wa Halmashauri walikuwepo. Hata hivyo, wananchi walichukua hatua ya kumtoa fisi huyo ndani ya nyumba na kumshambulia hadi kufa. Askari walipofika eneo la tukio, walikuta fisi tayari ameuawa.”
“Baada ya tukio hilo, serikali imeamua kushiriki kwenye msiba wa watoto wawili waliopoteza maisha. Vilevile, tumeanza operesheni ya kuwinda fisi katika maeneo hayo ili wananchi wakae salama. Operesheni hiyo ilianza jana usiku na itaendelea mpaka hali itakapokuwa shwari zaidi. Hadi sasa, hakuna fisi mwingine aliyeripotiwa kuonekana.”amesema DC Mkude
Aidha, majeruhi sita wa tukio hilo wamesafirishwa hadi hospitali ya mkoa kwa matibabu zaidi. “kwa upande wa majeruhi sita, baada ya kuona hali zao si nzuri, tumewapa rufaa kwenda Hospitali ya Mkoa kwa matibabu sahihi na uangalizi wa madaktari bingwa. Lengo ni kuhakikisha wanarejea katika hali yao ya kawaida haraka iwezekanavyo.”
Mhe. Mkude ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari katika kipindi hiki ambapo wanyama wakali wameanza kuonekana karibu na makazi ya watu. “Ni muhimu watoto wawe nyumbani mara baada ya kutoka shuleni na kupewa majukumu yanayoweza kufanyika katika mazingira salama,” amesisitiza Mkude.
Operesheni ya kuwinda fisi wengine imeendelea, na hadi sasa hakuna mnyama mwingine aliyeripotiwa kuonekana ambapo mazishi ya watoto waliofariki yanafanyika leo, huku serikali ikishirikiana na familia ya marehemu kuhakikisha taratibu zote zinaenda salama.
No comments:
Post a Comment