WIZARA YA NISHATI YAFANYA MAZUNGUMZO NA KAMPUNI YA EQUINOR TANZANIA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 9 November 2024

WIZARA YA NISHATI YAFANYA MAZUNGUMZO NA KAMPUNI YA EQUINOR TANZANIA







Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt.James Mataragio (tatu kulia) akiongoza kikao kati ya Wizara na Kampuni ya Equinor Tanzania AS. Kikao hicho kilifanyika hivi karibuni Jijini Cape Town wakati wa Mkutano wa Wiki ya Nishati Afrika.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt.James Mataragio (tatu kulia) akiongoza kikao kati ya Wizara na Kampuni ya Equinor Tanzania AS. Kikao hicho kilifanyika hivi karibuni Jijini Cape Town wakati wa Mkutano wa Wiki ya Nishati Afrika.

………………

*Wazungumzia uendelezaji wa Mradi wa LNG

Wizara ya Nishati imekutana na kufanya mazungumzo na Kampuni ya Equinor Tanzania AS kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Kusindika Gesi Asilia (LNG) pamoja na masuala mengine yanayohusu Gesi Asilia nchini.

Mazungumzo hayo yalifanyika hivi karibuni Jijini Cape Town – Afrika Kusini wakati wa Mkutano wa Wiki ya Nishati Afrika, mkutano ulioleta pamoja wadau zaidi ya 5000 kutoka ndani na nje ya Afrika.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio alisema kuwa Wizara ipo tayari kusikiliza na kuchukua mapendekezo yatakayotolewa na kampuni hiyo yanayolenga kuwezesha utekelezaji wa mradi kwa wakati.

“Niishukuru Equinor Tanzania kwa kuomba kikao hiki muhimu na Wizara. Tunatambua kuwa utekelezaji wa mradi huo wa kusindika gesi asilia unahusisha wadau wengine ambao hawapo hapa ila hiyo haizuii Wizara kukutana na kumsikiliza mdau mmoja mmoja kwani lengo letu ni kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa ufanisi.” alisema Mataragio.

Ujumbe wa Equinor uliongozwa na Makamu wa Rais wa Equinor Kanda ya Bara la Afrika, Bi. Nina Birgitte ambaye pamoja na kueleza masuala ya LNG na kutoa ushauri kwa Wizara, alitumia fursa hiyo kutoa taarifa ya mabadiliko ya uongozi wa juu wa kampuni hiyo nchini Tanzania ambapo alisema nafasi ya Maneja wa Equinor Tanzania ambayo kwa sasa inashikiliwa na Dr. Unni Fjaer itachukuliwa na Bi. Hilde Nafstad kutoka Norway.

Kampuni ya Equinor Tanzania AS ni miongoni mwa wabia wanaohusika katika utekelezaji wa mradi wa LNG nchini Tanzania.

Mradi huo unaolenga kuendeleza gesi asilia iliyogunduliwa katika kina kirefu cha Bahari ya Hindi Kusini mwa Tanzania, unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani takribani Bilioni 42.

Viongozi wengine kutoka Tanzania waliohudhuria kikao hicho ni Kamishna Msaidizi wa Petroli, Mha. Joyce Kisamo, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mha. Charles Sangweni na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Bw. Mussa Makame.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso