Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amekabidhi vifaa vya kilimo (Trekta za Mikono 12 ) zilizotolewa na Benki ya NBC Tawi la Shinyanga ambazo wamekabidhiwa wakulima 12 kutoka Kata ya Masengwa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga huku akiwashukuru na kuwapongeza sana Benki ya NBC kwa ubunifu wao huu wa kukopesha wakulima tena wa kawaida kabisa kwa vigezo rahisi na rafiki sana.
RC Macha amekabidhi na kusisitiza hayo tarehe 16 Novemba, 2024 katika hafla fupi iliyofanyika mbele ya jengo la NBC Benki tukio ambalo liliratibiwa, kusimamiwa na kutekelezwa vema na Meneja wa Tawi hili Bi. Joyce Chagonja na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Wakili, Julius Mtatiro.
Wengine waliohudhuria ni pamoja na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ndg. Edward Ngelela, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhe. Ngassa Mboje, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ndg. David Rwazo, wakulima na watumishi wa NBC Bank na wananchi ambapo amewataka wakulima kwenda kujiorodhesha katika maeneo yao ili waweze kutambulika na kuwa rahisi kunufaika pindi fursa zinapojitokeza.
"Kwa dhati kabisa nawapongeza sana Benki ya NBC Tawi la Shinyanga kupitia kwa Meneja wake Bi. Joyce Chagonja kwa muendelezo huu wa kutoa mikopo ya vifaa vya kilimo kwa wakulima wetu hasa hawa wa kawaida kabisa, hakika mmedhihirisha kuwa inawezekana kwa mkulima kupata mkopo huu tena kwa vigezo rahisi na rafiki ambavyo mkulima yeyote anawezamudu kuwa navyo, hongereni sana," amesema RC Macha.
Kwa upande wake Meneja wa Benki ya NBC Tawi Bi. Joyce amesema kuwa baadhi ya vigezo ni mkulima kuwa na shamba, kutambulika na uongozi wa kitongoji/kijiji, anayetumia mifumo ya kibenki katika kuuza mazao yake, awe mkulima wa zaidi ya miaka mitatu au zaidi, shamba lenye ukubwa wa hekari 10 au zaidi, awe anatambulika na Chama cha Ushirika huku akisisitiza kuwa huu ni mwendelezo wa mikopo ya vifaa vya kilimo lengo ni kuwawezesha kuwa na kilimo cha kisasa na chenye tija zaidi kwao.
@nbc_tanzania
@shinyangadc_official
#uchaguziserikalizamitaa2024
#shinyanga_rs
No comments:
Post a Comment