📌 *Serikali yajikita kufanya maboresho ya miundombinu ya umeme kukidhi mahitaji*
📌 *Kituo umeme Kinyerezi chafanyiwa upanuzi; chafungwa Transfoma za MVA 175*
📌 *Zanzibar kunufaika na maboresho hayo*
Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga amesema ukuaji wa kasi wa maendeleo na uchumi katika Mkoa wa Dar es Salaam unachangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa ongezeko la mahitaji ya umeme.
Ameyasema hayo leo 18 Novemba, 2024 wakati wa ziara yake kwenye Kituo cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi jijini Dar es Salaam iliyolenga kukagua maendeleo ya maboresho ya miundombinu ya umeme katika kituo hicho ili kukiongezea uwezo.
Kituo hicho kinachohudumia wakazi wa Gongo la Mboto, Mbagala, Kigamboni na Dege kinafungwa Transfoma yenye uwezo wa jumla ya 400 MVA huku Transfoma za ukubwa wa 175 MVA zikiwa zimeshafungwa.
‘’Nipende kuwatoa hofu wakazi wa Dar es Salaam na Pwani hususani Gongo la Mboto, Dege na Mkuranga kuwa TANESCO imekamilisha maboresho iliyokuwa ikifanya siku tatu zilizopita na tayari transfoma zimefungwa na hivyo kupunguza mzigo kwenye vituo vya Mbagala Ubungo na Dege na Gongo la Mboto‘’. Amesema Mhe. Kapinga
Ameeleza kuwa, kwa sasa kasi ya ukuaji wa Mkoa wa Dar es salaam ni takriban asilimia 16 huku mahitaji ya umeme yakiongezeka kutokana na shughuli za kiuchumi na ndio maana TANESCO imekuja na mpango wa maboresho ya miundombinu pamoja na njia za kusafirisha umeme ili kukidhi mahitaji ambapo kwa sasa tayari miradi kadhaa inaendelea kutekelezwa.
‘’ Lengo letu ni kuhakikisha Watazania hawakosi umeme kwenye kipindi chote cha maboresho kwani tunao umeme wa kutosha ili kukabiliana na kasi ya ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi na Viwanda.’’ Amesema Mhe. Kapinga
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mha. Gissima Nyamo-Hanga amesema hatua zinazochukuliwa kuboresha hali hiyo ni pamoja na kuboresha njia ya kusafirisha umeme msongo wa kikovoti 220 kutoka Kimara-Ubungo-Mabibo hadi Ilala na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Mabibo ili kupunguza mzigo kwenye kituo cha Ilala sambamba na kuboresha njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa Kilovoti 220 kutoka Ubungo hadi Ununio na hivyo kunufaisha pia Zanzibar.
Mkoa wa Dar es Salaam unapata umeme kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo Gesi Asilia ambapo mahitaji ya umeme ni wastani wa Megawati 602 huku Mkoa wa Pwani mahitaji yakiwa Megawati 136 na hivyo kufanya ukanda wote wa Pwani na Dar es Salaam kuwa na mahitaji ya megawati 738.
No comments:
Post a Comment