NA NEEMA NKUMBI - HUHESO DIGITAL USHETU
Katika baraza la madiwani lililofanyika Novemba 8, 2024, madiwani wa Halmashauri ya Ushetu wamelalamikia changamoto ya maji yenye chumvi yanayotokana na miradi ya visima vilivyochimbwa, na kuathiri matumizi ya maji kwa wananchi.
Madiwani wamesisitiza kuwa maji hayo yana chumvi nyingi na hayatumiki, hali inayowalazimu wananchi kununua maji kutoka kwa vyanzo vingine kwa gharama kubwa.
Diwani wa Kata ya Idahina, Mhe. Mathias Makashi ameeleza kwamba mradi wa maji wa kijiji cha Mwabomba unatoa maji yenye chumvi, na hivyo wananchi wamelazimika kununua maji ya lita ishirini kwa shilingi 500, ukilinganisha na bei ya maji kutoka kwenye mradi huo ya shilingi 50 kwa lita ishirini.
Mhe. Mathias amesema changamoto hii imekuwa ikijulikana tangu mwanzo, lakini hata hivyo, juhudi za kurekebisha hali hiyo bado hazijawa na mafanikio.
Mhe. Mathias ameshauri RUWASA kutafuta suluhisho la kudumu kwa tatizo hili, akiongeza kuwa wananchi wameelimishwa kuhusu matumizi ya maji ya miradi, lakini bado changamoto ya chumvi inawazuia kuyatumia.
Pia, diwani wa Kata ya Igunda, Mhe. Tabu Katoto, amelalamikia tatizo la mabomba kupasuka mara kwa mara, jambo linalosababisha upotevu wa maji na kuleta hasara kwa serikali.
Meneja wa RUWASA Kahama, Mhandisi Mkama Msilanga, akijibu maswali ya madiwani amesema kuwa kabla ya miradi kuanzishwa, hufanywa utafiti wa maji ili kuona kama yanafaa kwa matumizi ya binadamu ambapo ameeleza kuwa maji yenye chumvi ni matokeo ya miamba ya chini ya ardhi na kwamba maji hayo hayana madhara kwa binadamu.
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani, Mhe. Emanuel Makashi amesisitiza kuwa ni jukumu la RUWASA kutafuta sababu ya wananchi kuyakataa maji ya miradi na kutatua changamoto ya mabomba kupasuka, kwani upotevu wa maji unaleta hasara kubwa.
Mwenyekiti wa Baraza, Mhe. Gagi Lala amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa miradi kwa wakati, akiongeza kuwa wananchi wanapozungumzia matatizo yao ni wazi kwamba wanatarajia ufumbuzi wa haraka kwa changamoto walizozieleza.
Mbunge wa jimbo la Ushetu Mheshimiwa Emanuel Peter Cherehan akiwa katika baraza la madiwani Yshetu lililofanyika novemba 8, 2024
Madiwani wa halmashauri ya ushetu wakiwa katika baraza la madiwani lililofanyika novemba 8, 2024
Mwenyekiti wa Baraza, Mhe. Gagi Lala, akisisitiza umuhimu wa utekelezaji wa miradi kwa wakati, ili kukidhi matarajio ya wananchi na kutatua changamoto zao.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu, Hadija Mohamed KABOJELA ambaye ni katibu wa baraza la madiwani ushetu
No comments:
Post a Comment