NA NEEMA NKUMBI -KAHAMA
Bank ya NMB imezindua rasmi kampeni yao ya kila mwaka ya Bonge la Mpango, ikiwa na lengo la kuwahamasisha wateja kujiwekea akiba katika akaunti zao.
Katika uzinduzi uliofanyika leo, Novemba 28, 2024, Wilayani Kahama, Meneja wa Kanda ya Magharibi wa Benki ya NMB, Renatus Assenga, alieleza kuwa kampeni hiyo inalenga kusaidia wananchi kuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba, ili kuwaepusha na mikopo yenye riba kubwa wakati wanapokutana na changamoto za kifedha.
Assenga amefafanua kuwa mshindi wa jumla katika kampeni hii atapata kitita cha shilingi milioni mia moja (100,000,000 TZS) taslimu, Aidha, amesema kuwa kila wiki kutakuwa na washindi kumi watakaojishindia shilingi laki moja (100,000 TZS) kila mmoja, pamoja na zawadi nyingine za manufaa ikiwemo friji, simu za kisasa (smartphones), TV, mashine ya kufulia na gesi.
"Tumekabidhi zawadi kwa washindi leo, ambapo Benard Kimario ameshinda trekta la kilimo (powertiller) na Chausiku Jindiga ameshinda microwave," amesema Assenga.
Kampeni hiyo inaendelea kwa zaidi ya wiki 12 kuanzia leo na zaidi ya washindi watatu wamepatikana kupitia droo, ambapo zawadi zao zitakabidhiwa hivi karibuni.
Kwa upande wake, Benard Kimario, ambaye ameshinda trekta la kilimo, amesema kuwa zawadi hiyo itamsaidia sana katika shughuli zake za kilimo, na ametoa shukrani kwa Bank ya NMB kwa kuanzisha kampeni inayosaidia kuboresha maisha ya wananchi.
NMB inaendelea na juhudi za kutoa motisha kwa wateja wake, huku ikiwahimiza kujiwekea akiba na kujiunga na huduma za kifedha ambazo zitawawezesha kufikia malengo yao ya kifedha.
No comments:
Post a Comment