*Kuelekea Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania 2024*
*Na Wizara ya Madini*
*Ukiuza Madini Nje ya Soko wewe ni mtoroshaji*
Tulikuwa na changamoto ya biashara ya Madini kabla ya mwaka 2017 ambapo ilifanyika kiholela kutokana na kukosekana kwa masoko ya madini. Hivi sasa biashara yote inafanyika sokoni, ukiuzia nje ya Soko wewe ni mtoroshaji unakiuka Sheria za nchi na kupoteza mapato ya Serikali.
*Tozo kwenye uchimbaji mdogo*
Nimefanya vikao na wadau mbalimbali kusikiliza hoja zao lengo ni kuangalia namna ya kutatua changamoto kwenye shughuli za uchimbaji mdogo wa madini na biashara ya madini. Hivi sasa kodi zote zinazolipwa Serikalini zimebaki asilimia 9.3 kutoka 38. Mrabaha ni asilimia 6, ada ya ukaguzi asilimia1, TRA asilimia 2 (withholding tax) na Service levy asilimia 0.3. Serikali imechukua hatua kubwa kusikiliza changamoto za wachimbaji wadogo, kodi inayokusanywa inasaidia kujenga nchi yetu.
*Mkakati wa Kuongeza Thamani Madini Nchini*
Kwenye hotuba yangu ya Bajeti nilieleza kuhusu mpango wa Serikali kutoendelea kutoa Leseni za uchimbaji mkubwa wa madini kama mwekezaji haleti mpango unaoridhisha wa uongezaji thamani madini. Uongezaji thamani madini unalenga kubakiza ajira nchini, ujuzi na kuongeza mapato ya nchi yetu. Suala hili kwenye Mkutano wetu wa Uwekezaji utakaofanyika tarehe 19-21 Novemba, 2024, ni jambo ambalo linakwenda kuubeba mkutano wetu.
*Tanzania kuwa Kinara wa Madini Afrika Mashariki na Kati*
Kupitia Kiwanda cha Kusafisha madini ya metali kitakachojengwa Buzwagi Kahama na Kampuni ya Tembo Nikeli kutaifanya Tanzania kuwa kinara katika uongezaji thamani madini kupitia kiwanda hicho ambacho mtaji wake ni Dola za Marekani Milioni 500. Mradi huu utakuwa ni fursa kubwa kwa Tanzania kujitangaza.
*STAMICO na Soko la Hisa*
Tumewapa leseni za utafiti Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) tunataka taarifa zao wazipeleke Toronto, London Exchange market, niliwaambia STAMICO nataka niwaone wakishindana na kampuni kubwa kama Barrick na GGML. STAMICO ni shirika lililokuwa linakwenda kufa lakini sasa hivi shirika hili linafanya vizuri sana. Shirika hili limetoka kukusanya shilingi bilioni 2 hadi bilioni 80.
*Megawati Elfu Mbili za Makaa ya Mawe*
Tuna mradi mkubwa wa kuchimba makaa ya mawe Kiwira unaofanywa na STAMICO. Tumeanza majadiliano na kampuni moja ya India yakienda vizuri kupitia mradi huo tutazalisha megawati za umeme Elfu Mbili kupitia makaa ya mawe.
*Mpango wa kuwainua wachimbaji wadogo*
Nataka nione wachimbaji wadogo wana graduate kutoka kwenye uchimbaji mdogo kwenda wa Kati. kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) tumenunua mitambo 15. tayari tumepokea mitambo Mitano (5), na imekwishaanza kazi kwa ajili ya shughuli za uchorongaji ili kuwasaidia kupata taarifa za sahihi.
*Kuwaendeleza wachimbaji wadogo*
Kupitia vituo vyetu vya mfano vya Lwamgasa Geita, Katente-Geita na Chunya, tunawaandaa wachimbaji kutumia teknolojia rahisi ili kuachana na matumizi ya zebaki. Tumefunga mitambo ya kuchenjua dhahabu kubadili mtazamo wa matumizi ya zebaki hivi sasa wachimbaji wengi wameanza kufunga mitambo hiyo. Leo nina furaha kubwa kati ya shilingi bilioni 753 zilizokusanywa Mwaka wa Fedha 2023/24, asilimia 40 imechanganyiwa na wachimbaji wadogo.
*Mkaa wa Kupikia wa Rafiki Briquettes*
Tunatengeneza mkaa wa kupikia wa Rafiki Briquettes unaotokana na makaa ya mawe, ulianza kama majaribio na tayari hivi sasa wamefunga mashine mbili na wameanza kutafuta mawakala.
*Liganga na Mchuchuma*
Mradi huu umekuwa na historia ndefu na kilio cha watanzania wengi ni kutaka mradi huu uanze. Hivi sasa tuko kwenye hatua nzuri na tayari fidia zimekwishalipwa.
*Shilingi Bilioni 115 zimeelekezwa kwenye Utafiti wa Madini*
Katika Mwaka wa fedha 2024/25 tumepanga kununua helicopter itakayofungwa vifaa kwa ajili ya shughuli za utafiti wa madini. Utafiti ni moja ya kazi zinazotumia gharama kubwa sana, Napenda kumshukuru Mhe. Rais Samia kwa sababu kwa mwaka huu wa fedha Bajeti ya Wizara imeongezeka kufikia shilingi bilioni 231 huku shilingi bilioni 115 ni fedha za maendeleo kwa ajili ya utafiti.
*#TMIC2024*
*#ValueAdditionForSocioEconomic*
*#InvestInTanzaniaMiningSector*
*#UongezajiThamaniMadiniKwaMaendeleoYaKiuchumiNaKijamii*
*#Vision2030:* *#MadiniNiMaishaNaUtajiri*
No comments:
Post a Comment