Na. Elimu ya Afya kwa Umma.
Leo Oktoba 4, 2024 Wizara ya Afya imetoa mafuzo kwa Waandishi wa habari na Wahariri kutoka vyombo vya habari mbalimbali Nchini kuhusu ugonjwa wa Mpox na Marburg ili kuweza kutoa elimu kwa jamii namna ya kujikinga na kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa hayo.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma Dkt. Ona Machangu amewataka wahariri na waandishi wa habari kutumia taaluma zao kuweza kuifikishia jamii elimu na hamasa juu ya kujikinga na magonjwa hayo ya mlipuko.
"Wanahabari na Wahariri wote tuendelee kushirikiana na Wizara ya Afya na kujenga mahusiano mazuri ili tuweze kuikinga jamii yetu dhidi ya magonjwa haya ya mlipuko, tuelimishe na kuhamasisha jamii kuweza kufuata hatua mbalimbali za kujikinga kama kunawa mikono kwa maji safi na sabuni, kuepuka kushikana mikono na njia nyingine za kujikinga na magonjwa haya", amesema Dkt. Ona
Aidha Dkt. Ona ameitaka jamii kuendelea kujikinga na kuchukua tahadhari zote muhimu ili kujikinga na magonjwa hayo kwani tayari baadhi ya nchi za jirani zina maambukizi ya magonjwa hayo.
Pia ameitaka jamii kuwa na utaratibu wa kufika katika vituo vya afya na kutoa taarifa kwa watoa huduma za afya waonapo dalili za magonjwa hayo kama kutokwa na vipele mwilini, kuchoka mwili, kutoka na damu puani au masikioni pamoja na dalili nyingize za magonjwa hayo ili watoa huduma wa afya waweze kumpatia matibabu.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Afya Bw. Englibert Kayombo amesema kuwa semina hiyo ya waandishi wa habari ni endelevu na taratibu za Wizara kukaa pamoja na wadau hao ili kuwapa elimu muhimu itayawasaidia katika kutoa taarifa kwa usahihi.
Naye James Mhilu, Mratibu wa Mafunzo hayo amewataka Waandishi wa habari na Wahariri kuwakumbusha wananchi kupiga namba 199 kituo cha miito ya simu cha Wizara ya Afya (Afya Call Center) kwa taarifa, maoni na ushauri zaidi.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu alipotembelea uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar Es Salaam Oktoba 1, 2024, alibainisha kuwa Tanzania ni salama na hakuna mgonjwa yeyote aliyethibishwa kuwa na maambukizi ya Ugonjwa wa Mpox wala Marburg nchini.
Dkt. Jingu alibainisha kuwa Serikali kwakushirikiana na wadau wa Sekta inajikita zaidi kwenye utoaji wa elimu na hamasa kwa jamii ili waweze kujikinga dhidi ya magonjwa hayo ya mlipuko na waweze kutoa taarifa haraka kwa mamlaka husika endapo watabaini uwepo wa mtu mwenye dalili za magonjwa hayo.
Semina hii kwa wanahabari ni jitihada mojawapo zinazochukuliwa na Wizara ya Afya katika kufikia jamii kupitia waandishi wa habari ambao sasa wamewezeshwa na elimu muhimu kuhusu magonjwa ya Mpox na Marburg.
No comments:
Post a Comment