WAZIRI MKUU ASEMA LISHE BORA NI KIPAUMBELE CHA SERIKALI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Thursday 3 October 2024

WAZIRI MKUU ASEMA LISHE BORA NI KIPAUMBELE CHA SERIKALI




WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa suala ya lishe ni kipaumbele muhimu kwa Serikali katika kuwezesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo na shughuli za kiuchumi kwa jamii jamii zikiwemo za kilimo, uvuvi, ufugaji na biashara.



Amesema hayo leo (Alhamisi, Oktoba 03, 2024) wakati alipofunga Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe kwenye ukumbi wa Malaika Beach Resort jijini Mwanza.



Amesema kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kutokomeza aina zote za utapiamlo nchini. “Mheshimiwa Rais Dkt. Samia amedhihirisha dhamira yake ya dhati ya kulipa umuhimu wa kipekee suala la lishe.



Hatua ambayo imemfanya awe kinara na mmoja wa viongozi wanaotambuliwa na kutolewa mfano ulimwenguni kwa hatua ambazo wameweza kupiga katika mapambano dhidi ya changamoto za utapiamlo”



Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wadau wote wa lishe wahakikishe wanatumia vizuri matokea ya ripoti ya mapitio ya muda wa kati ili kujitathmini na kuchukua hatua stahiki za kuboresha utekelezaji wa afua za lishe.



Pia, Waziri Mkuu ameziagiza mikoa na halmashauri zote nchini itumie mwongozo wa Kitaifa wa utoaji wa huduma ya chakula na lishe kwa wanafunzi wa elimu ya msingi na wahakikishe matumizi ya vyakula vilivyorutubishwa yanajumuishwa na kutengewa fedha katika mipango na bajeti za kila mwaka.



“Ofisi ya Rais - TAMISEMI hakikisheni kuwa mikataba ya lishe kati ya Mheshimiwa Rais na Wakuu wa Mikoa inatekelezwa kikamilifu na kuwa na tija. Endeleeni kufanya ufuatiliaji wa karibu na kutoa taarifa za utekelezaji mara kwa mara.”



Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka wizara, wakala, taasisi na mashirika ya umma watumie kikamilifu mwongozo wa mpango jumuishi wa Taifa wa lishe na bajeti na kuhakikisha masuala ya lishe yanajumuishwa katika mipango na kutengewa fedha ili yatekelezwe kikamilifu kila mwaka.



Kwa Upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi amesema kuwa mkutano huo umekutanisha wadau wa lishe wanaotekeleza masuala ya lishe kutoka sekta za umma, binafsi na washirika wa maendeleo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso