UJENZI WA BARABARA ZA MRADI WA DMDP AWAMU YA PILI UTALETA MABADILIKO CHANYA MKOANI DAR ES SALAAM - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday 26 October 2024

UJENZI WA BARABARA ZA MRADI WA DMDP AWAMU YA PILI UTALETA MABADILIKO CHANYA MKOANI DAR ES SALAAM


Na. James K. Mwanamyoto OR-TAMISEMI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II) utaleta mabadiliko chanya katika ujenzi wa miundombinu ya barabara katika Mkoa wa Dar es Salaam, ikiwa ni zaidi ya mabadiliko yaliyoletwa na awamu ya kwanza ya mradi huo.


Waziri Mchengerwa amesema hayo leo jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Mwembe Yanga Temeke, wakati wa hafla ya utiaji saini wa mikataba ya awali ya ujenzi wa zaidi ya kilomita 168.22 za barabara za Mkoa wa Dar es Salaam zitakazojengwa na mradi wa DMDP awamu ya 2.


Mhe. Mchengerwa amesema kuwa, jumla ya zabuni 19 tayari zimeshatangazwa na zipo katika hatua mbalimbali za manunuzi ili utekelezeji wa miradi ya DMDP awamu ya pili uanze maramoja.


“Kati ya zabuni hizo 19 zilizotangazwa, leo tumeshuhudia utiaji saini wa mikataba 8 ya awali yenye thamani ya Shilingi 190,040,361,931.41 ambayo itajenga jumla ya kilomita 63.66 za barabara katika mkoa wa Dar es Salaam,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.


Waziri Mchengerwa amesema, ujenzi wa barabara hizo unadhihirisha kuwa Serikali ina nia ya dhati ya kuboresha maisha ya wananchi wa Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na kuboresha muonekano wa Jiji la Dar es Salaam.


Aidha, Mhe. Mchengerwa amemtaka Katibu Mkuu-TAMISEMI Bw. Adolf Ndunguru kushirikiana na Mtendaji Mkuu wa TARURA ili kuhakikisha utekelezaji wa mikataba hii unafanyika kwa ufanisi mkubwa kama ilivyofanyika katika awamu ya kwanza, hali iliyopelekea wabia wa maendeleo kutoa fedha za kutekeleza awamu ya pili ya mradi wa DMDP.


Malengo ya Serikali kupitia utekelezaji wa mradi wa DMDP awamu ya 2 ni kuboresha miundombinu ya msingi katika Halmashauri zote za Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na kuzijengea uwezo wa utoaji huduma bora kwa wananchi.


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso