📌 *Kuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa 216,000 kwa siku*
📌 *Ujenzi wa kiwanda cha kuweka mfumo wa joto kwenye mabomba wafikia 92%*
*Vijiji 12,240 vyafikiwa na nishati ya umeme*
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mussa Makame amesema utekelezaji wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki ( EACOP), umefikia asilimia 43.5 huku baadhi ya kazi za ujenzi katika makambi na vituo vya kuhifadhia mabomba zikikamilika kwa asilimia 100.
Amesema hayo leo wakati akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga, Tanzania.
"Kazi za mradi wa EACOP zinahusisha ujenzi wa bomba la urefu wa kilomita 1,443 na miundombinu mingine huku kilomita 1,147 sawa na asilimia 80 zikiwa upande wa Tanzania." Amesema Makame
Ameeleza kuwa, ujenzi wa kiwanda cha kuweka mfumo wa joto kwenye mabomba (thermal Insulation System Plant - TIS) umefikia asilimia 92.
Ameongeza kuwa, bomba litapita katika Mikoa nane ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.
Amesema bomba hilo la kusafirisha mafuta ghafi litakuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa 216,000 ya mafuta ghafi kwa siku.
Kamati hiyo ya Bunge pia imepokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme Vijijini, Vijiji-Miji na kwenye maeneo ya Viwanda vidogo katika Mikoa ya Ruvuma, Njombe, Mbeya na Rukwa.
Mkurugenzi Mkuu, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy ameieleza Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa hadi kufikia Septemba 2024 jumla ya Vijiji 12,240 vimefikiwa na huduma ya umeme ambalo ni ongezeko la Vijiji 11,734 tangu mwaka 2007.
"Mafanikio mengine ni kuchangia uboreshaji wa huduma za jamii zikiwemo afya, elimu na maji maeneo ya Vijijini." Amesema Mhandisi Saidy
Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, Mha. Hassan amesema katika mwaka huu wa fedha Serikali itasambaza mitungi 450,000 kwa bei ya ruzuku kwa wananchi nchi nzima.
Kuhusu Mradi wa upelekaji umeme kwenye maeneo ya migodi midogo, viwanda na maeneo ya kilimo katika Mikoa ya Ruvuma, Njombe, Mbeya na Rukwa, Mha. Saidy amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa kilometa 1,372.39 za umeme wa msongo wa kati, Kilomita 995.81 za umeme msongo mdogo, ufungaji wa transfoma 603 na uunganishwaji wa umeme kwenye maeneo 591
No comments:
Post a Comment