Na Paul Kayanda, Geita.
Mwenyekiti wa chama cha Wachimbaji wadogo Mkoa wa Geita (GEREME) Titus Kibuo na mwekezaji katika sekta ya madini mkoani Geita Titus Kabuo ameonyesha mfano kama kiongozi kwa kuchukua hatua ya kipekee ya kuingia ndani ya maduara yenye urefu wa mita 400 chini ya ardhi kwenye migodi yake ya dhahabu.
Kabuo, alichukua hatua hiyo ili kuhamasisha wafanyakazi wake kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura, Hatua hiyo inalenga kuwapa wafanyakazi wake nafasi ya kushiriki kikamilifu katika michakato ya kidemokrasia ya nchi yao, jambo linaloweza kuleta mabadiliko chanya kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari alioambatana naye kwa wafanyakazi wa mgodi huo, Kabuo alisisitiza umuhimu wa kila raia kutumia haki yake ya kidemokrasia kwa kujiandikisha kupiga kura.
"Sisi sote tuna wajibu wa kuhakikisha kuwa sauti zetu zinasikika katika masuala muhimu ya kitaifa, na njia pekee ya kufanya hivyo ni kwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi hakikisheni mnawahi katika vituo vya kujiandikishia." Alisema Kabuo.
Alieleza kuwa kura ni zana muhimu kwa raia kuleta mabadiliko, na kila mmoja ana jukumu la kuhakikisha kuwa anachangia katika mustakabali wa taifa.
Kibuo pia aliongeza kuwa kujiandikisha kupiga kura si tu haki bali ni wajibu wa kila mfanyakazi na raia wa Tanzania. Kwa kufanya hivyo, anatarajia kuwa wafanyakazi wake watachangia katika kuleta mabadiliko yanayohitajika, sio tu katika sekta ya madini bali pia katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
"Sote tunatamani kuona nchi yetu ikipiga hatua kubwa za maendeleo, lakini maendeleo hayo hayaji bila sisi kushiriki katika maamuzi muhimu ya kitaifa," aliongeza Kibuo.
Aidha, mwenyekiti huyo amewahimiza wafanyakazi wake kuona ushiriki wao katika uchaguzi kama fursa ya kuboresha hali zao za maisha, kwani viongozi wanaochaguliwa wana uwezo wa kubuni sera zitakazoleta mabadiliko katika sekta ya madini na maeneo mengine ya uchumi.
Kabuo anaamini kuwa ushiriki wa kila mmoja kwenye mchakato wa kidemokrasia ni nguzo muhimu ya maendeleo endelevu ya taifa.
Hatua ya Kibuo imepokelewa kwa shangwe na wafanyakazi, ambao wamesifu jitihada zake za kuwahamasisha kushiriki katika uchaguzi.
Wengi wao wamesema kwamba hawakujua umuhimu wa kujiandikisha kupiga kura, lakini kutokana na mwongozo wa Kibuo, sasa wanaelewa vizuri zaidi umuhimu wa haki yao ya kidemokrasia.
Kwa Kabuo, hili ni jukumu la kitaifa na kijamii, na ameahidi kuendelea kuhamasisha ushiriki wa wafanyakazi wake katika masuala yote muhimu ya kitaifa.
No comments:
Post a Comment