WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza wa Mpango mkakati wa miaka mitano 2024/25 – 2029/30 wa Anga za juu utakaoiwezesha Tanzania kurusha satelaiti.
Amesema kuwa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam imepata mradi wa Utafiti wa kuwezesha urushaji wa satelaiti unaosimamiwa na Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya anga za juu ikishirikiana na Taasisi ya Anga za Juu ya Japan (JAXA).
Amesema hayo leo (Alhamisi Oktoba 17, 2024) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kilele cha Kongamano la Nane la Mwaka la TEHAMA, lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.
“Katika eneo hili Maandalizi ya utungwaji wa Sera, Sheria na uridhiwaji wa mikataba ya Kimataifa ya masuala ya anga za juu inaendelea”.
Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iwakusanye vijana wabunifu wenye uwezo wa kubuni teknolojia zenye manufaa kwa Taifa “Lakini simamieni hizi tafiti zenye kutoa matokeo na vijana hao waendelee kupewa fursa na kazi hizo ziingie kwa jamii na zianze kutumika”
Pia Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Wizara ya Mawasiliano, Habari na Teknolojia ya Habari isimamie na kuhakikisha ujenzi wa Vituo vya Ubunifu (Innovation Hubs) katika mikoa iliyokubalika unafanyika kama ilivyopangwa.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa mabadiliko ya kidijitali ni lazima na Safari hiyo haipaswi kumuacha mtu yeyote nyuma hususan kwenye mfumo wa kifedha jumuishi. “Kama mnakumbuka, Serikali katika mwaka 2020 ilizindua Mfumo wa N-Card ambao hadi kufikia sasa umefanikiwa kuwaunganisha wananchi wasiopungua milioni nne. Mfumo huo umesaidia sana kuokoa upotevu wa fedha katika vituo vya usafirishaji”
Ameongeza kuwa mfumo huo umesaidia kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato. “Nitoe wito kwa Wizara kuhakikisha maeneo mengi ambayo Serikali imewekeza yanatumia mfumo wa N-card. Mfumo huo ni muhimu katika kuokoa upotevu wa fedha za Serikali na kuwasaidia wananchi kuacha kutembea na fedha taslimu na watumiefedha kwa njia ya kidijitali”
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Wizara ya Mawasiliano, Habari na Teknolojia ya Habari ihamasishe matumizi ya TEHAMA katika kutoa huduma, biashara na uzalishaji ili kuongeza uwazi, ufanisi na kuboresha maisha ya wananchi kiuchumi na kijamii;
No comments:
Post a Comment