WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haijatoa maagizo ya kuwaondoa kazini walimu wa cheti bali amewataka watumie mpango wa mafunzo endelevu kazini kwenda vyuoni kusoma.
Amesema Serikali imefanya maboresho ya sera na mitaala ya elimu nchini ambayo pamoja na mambo mengine imeleta mabadiliko katika sifa za chini za mwalimu katika shule za msingi kuwa Stashahada/Diploma. “Pamoja na mabadiliko haya, Serikali inatambua kuwa bado wapo walimu ambao hawajafikia sifa ya kuwa na Astashahada au Diploma na hakuna agizo la kuwataka waondolewe katika ajira,” amesema.
Amesema walimu wote ambao hawana sifa ya Astashahada au Diploma watumie fursa ya mpango wa mafunzo endelevu kazini kwenda vyuoni kusoma ili kupata sifa ya diploma au kujiendeleza kupitia moduli kwa mfumo wa LMs - Learning Management Systemchini ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE).
Akielezea kuhusu upandishaji madaraja kwa walimu, amesema: “Kati ya Machi, 2021 na Agosti, 2024, walimu 601,698 nchi nzima wamepandishwa madaraja na Serikali imetumia shilingi trilioni 1.3 kuwalipa. Na niwatake Maafisa Elimu kuwatembelea walimu vijijini na kusikiliza kero zao,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Amesema katika kipindi cha kuanzia Machi, 2021 hadi sasa, Serikali imeweza kuwabadilisha kada/miundo jumla ya watumishi 36,768 kwa gharama ya sh. 3,090,476,931.00 na imelipa madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi 144,356 yenye jumla ya sh. milioni 229.9.
Akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadhara hiyo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewashukuru walimu wa Tanzania kwa kuendelea kuiheshimisha taaluma yao na kuwa chanzo cha maarifa kwao hakitoki kwingine isipokuwa kwao hivyo wailinde kwa wivu mkubwa taaluma hiyo.
Dkt. Biteko amesema mwaka 2015 wakati anachaguliwa kuwa Mbunge, wilaya yake ilikuwa ikishika nafasi ya mwisho katika mitihani ya Taifa. “Nilizungumza na walimu kuhusu matokeo mabaya na wakasema tusiwaache walimu nyuma hivyo tulianza kukutana na kufanya tathimini na sasa tunafanya vizuri.”
No comments:
Post a Comment